Luis atoboa siri tishio la namba linavyompasua kichwa Simba

Monday March 23 2020

 

By Thobias Sebastian, Mwananchi

Wakati mashabiki wa Simba wakiamini Luis Miquissone ni mkombozi wao, winga huyo amesema ana changamoto ya kupigania namba kikosi cha kwanza.

Kiwango cha nyota huyo wa zamani wa UD Songo ya Msumbiji, kimewakuna mashabiki wa Simba na wanamuona ni Meddie Kagere mpya.

Licha ya kufunga mabao matatu akiachwa mbali na Kagere (19), Luis ameonyesha uwezo ambao Simba haiwezi kujuta kumsajili katika dirisha dogo la Januari, mwaka huu.

Luis alithibitisha ubora wake katika mchezo dhidi ya Yanga licha kufungwa bao 1-0. Kipa wa Yanga Metacha Mnata anakumbuka vyema kiki za winga huyo ambaye anatumia miguu yote miwili.

Akizungumza na Spoti Mikiki, mchezaji huyo anasema anataka kuifungia Simba mabao kwa kuwa ana kipaji cha kucheza soka ya ushindani.

“Simba wakati wananisajili nilikuwa katikati ya likizo baada ya msimu wa mashindano kumalizika natumia muda zaidi kufanya mazoezi ya nguvu ili kuwa fiti kimwili na kiakili .

Advertisement

“Naendelea kuimarika lakini bado sijafika pale ambapo natamni kujiona nacheza katika kiwango kama kile ambacho kiliwavutia Simba mpaka wakanisajili, siku si nyingi nitakuwa katika ubora huo,”anasema winga huyo.

Luis anasema licha ya kusajiliwa akitokea nje, lakini nafasi yake ya kiungo wa pembeni imekuwa na changamoto kubwa ya kupata namba kikosi cha kwanza.

Nafasi ya Luis ina wachezaji Shiza Kichuya, Ibrahim Ajibu, Cletous Chama, Hassan Dilunga, Deo Kanda, Rashid Juma na wengine kulingana na mahitaji ya kocha.

Luis anasema hawezi kubweteka kwa kuwa kazi yake ni soka atapambana kupata namba kikosi cha kwanza licha ya kuwepo changamoto.

“Nitapoteza nafasi kama nitafanya mzaha katika mechi au mazoezi hali haitakuwa nzuri kwangu kwasababu timu yetu ina wachezaji wengi hodari natakiwa kupambana kiushindani,” anasema Luis.

Pia anasema wachezaji wanaocheza ligi wanacheza vyema na wamekuwa na mchango mzuri kwa timu zao akiwemo Morrison wa Yanga.

“Wachezaji wanaocheza ligi ni hodari ndio maana tunacheza katika daraja moja, nadhani si sahihi kumzungumzia mchezaji fulani,” anasema Luis.

Anasema mabao matatu ambayo amefunga mpaka sasa katika ligi si kwamba atakuwa ameishia hapo kwani malengo yake ni kufunga mengi zaidi lakini awe amehusika katika mabao ambayo wamefunga wachezaji wengine kwa maana ya kutoa pasi za mwisho.

“Hata kama nimeingia katika timu kwenye dirisha dogo huku nikionekana kuwa bado sipo fiti najiona naweza kufunga mabao mengi zaidi ya hayo katika michezo ambayo imebaki lakini vile vile ni kuwa mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha timu yangu kwa maana ya kutoa mchango wa kutosha,” anasema.

Advertisement