Mabeki watano bora Ligi Kuu Bara

Kwa mtazamo wa haraka unaweza kuona Tanzania inakosa mabeki mahiri wa kati waliovuma kwa nyakati tofauti kwa ubora wao. Miongoni mwa majina makubwa yaliyotamba ni Jella Mtagwa, Mohammed Bakari ‘Tall’, Athumani Chama, Frank Kassanga ‘Bwalya’, George Masatu, David Rogers na wengine wengi tu.

Ingawa zama za akina Kassanga zimeondoka, Ligi Kuu msimu huu imewaibua mabeki watano wa kati ambao wanafanya vyema katika mashindano.

Iddi Mobi- Polisi Tanzania

Beki huyo msimu uliopita alikuwa alikuwa Mwadui na ndipo Polisi Tanzania ilipomuona na kumpa mkataba wa kucheza eneo la ulinzi.

Licha ya Polisi Tanzania kuwa timu ngeni kwenye Ligi Kuu lakini inabebwa na wachezaji mahiri iliyowasajili akiwemo Mobi ambaye amekuwa mhimili katika safu ya ulinzi.

Mobi, kijana mrefu, mweupe na mwenye umbo lililojaa amekuwa kikwazo kwa washambulaaji na ubora wake ulithibitika katika mechi dhidi ya Yanga Oktoba 3 iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Bakari Mwamnyeto- Coastal Union

Jina lake limetawala midomoni mwa mashabiki wengi baada ya kucheza kwa kiwango bora msimu huu.

Beki huyo ameonyesha uwezo mkubwa katika ligi na Taifa Stars ambapo alicheza kwa kiwango bora mechi mbili za kimataifa dhidi ya Rwanda na Sudan.

Mwamnyeto alionyesha kiwango bora dhidi ya Sudan Oktoba 10 na kuziba pengo la beki nyota nchini Kelvin Yondani ambaye alibaki Dar es Salaam kutokana na kuwa majeruhi.

Beki huyo ni hodari wa kuokoa mipira ya juu na chini lakini zaidi anatumia akili pale anapopambana na mshambuliaji wa timu pinzani.

Idadi kubwa ya makocha na wadau mbalimbali wanamtabiria makubwa Mwamnyeto kwamba huenda akawa ndiye mrithi wa Yondani katika kikosi cha Taifa Stars.

Pia si ajabu kusikia klabu kongwe za Simba na Yanga kuanza harakati za kumsajili kwa ajili ya msimu ujao kutokana na ubora wake anapocheza uwanjani.

Abdallah Mfuko- KMC

Amesajiliwa na KMC akitokea Ndanda lakini amekuwa akianza katika kikosi cha kwanza kutokana na uwezo mkubwa.

Ni mmoja wa mabeki ambao wamekuwa wakikaba kwa nguvu na huwa hana masihara na washambuliaji watukutu wenye uchu wa kufunga mabao.

Carlos Protas- Namungo

Moja ya sifa kubwa ya beki huyo wa Namungo ni kucheza kwa kutumia akili. Hana rekodi mbaya ya nidhamu kwa washambuliaji wa timu pinzani ni hodari wa kuruka kuokoa mipira ya kichwa.

Ingawa ina msimu mmoja katika ligi, Namungo imetoa ushindani katika mechi zake dhidi ya wapinzani wao.

Sadalah Lipangile - KMC

Nahodha msaidizi wa KMC ambaye ameendelea kucheza kwa kiwango bora katika mechi alizopangwa kwenye Ligi Kuu Bara.

Lipangile ana uwezo mzuri wa kucheza kwa ufanisi na amekuwa akicheza pacha katika safu ya uliniz na Abdallah Mfuko.

Haishangazi kocha Jackson Mayanja kutoa nafasi kwa mabeki hao kucheza pamoja katika safu ya ulinzi.

Beki huyo ana nafasi ya kucheza muda mrefu kutokana na umri wake kama ataendelea kuwa na nidhamu ya mchezo ndani na nje ya uwanja.

Ingawa wapo mabeki wengine waliocheza vyema katika mechi za msimu huu, lakini akina Mwamnyeto wameonyesha ni hazina kwa timu zao.

Huenda msimu ujao mabeki hao wakasajiliwa na klabu nyingine baada ya kucheza kwa kiwango bora msimu huu.