Breaking News

Usajili wa Simba, Yanga gumzo

Tuesday August 6 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Maandalizi ya msimu ujao wa 2019/2020 kwa kiasi kikubwa yamekamilika kwa vigogo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba na Yanga ambao walitumia dirisha lililofungwa la usajili kuimarisha vikosi vyao.

Baada ya kupata viongozi wapya, Yanga imeonekana kuwa na nguvu kifedha kwa kuwasajili wachezaji 14 wapya ambao ni Patrick Sibomana, Issa Bigirimana, Metacha Mnata, Farouk Shikalo.

Wengine ni Selemani Mustafa, Mapinduzi Balama, Lamine Molo, Muharami Issa ‘Marcelo’, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo, Juma Balinya, Ally Sonso, Ally Ally na David Molinga.

Simba wamesajili wachezaji wapya 11 ambao ni Miraji Athumani, Kennedy Juma, Tairone da Silva, Gerson Viera, Wilker da Silva, Francis Kahata, Deo Kanda, Sharaf Shiboub, Ibrahim Ajibu, Gadiel Michael na Beno Kakolanya.

Pamoja na timu hizo kusajili wachezaji wengi lakini hawa ndio wanaonekana kuwa wamebamba zaidi kwa mashabiki wa wengi wa soka nchini kutokana na viwango vyao bora kwa muda mrefu.

Ally Ally

Advertisement

Beki huyu ambaye uwezo wake ulionekana tangu akiwa na Stand United ya Shinyanga, wengi walitegemea huenda kutokana na uwezo wake angetimka klabuni hapo tangu mwaka juzi ambapo alifanya kazi kubwa katika mchezo dhidi ya Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa.

Ally aliendelea kulinda kiwango chake akiwa na ndoto ya siku moja kucheza moja ya klabu kubwa nchini ambapo katika usajili wa mwaka huu Yanga imemnasa beki huyo wa kati akitokea KMC akiwa na mwaka mmoja tu tangu alipotimka Stand United.

Beno Kakolanya

Kizuri chajiuza na Kibaya chajitembeza, hiyo ndiyo tafsiri ya haraka unayoweza kuitoa juu ya kipa huyo ambaye hakuna asiyefahamu ubora wake licha ya kuwa na mgogoro dhidi ya waajiri wake wa zamani Yanga.

Kipa huyo anayetajwa miongoni mwa makipa bora nchini amemaliza sintofahamu iliyokuwa ikiendelea juu ya mustakabali wake ndani ya klabu ya Yanga baada ya kutia saini mkataba wa miaka miwili kwa watani wao Simba.

Utakumbuka kipa huyo hakuwa katika kikosi kilichocheza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kutokana na mgogoro wa kifedha aliokuwa nao dhidi ya Yanga, hivyo wengi walihisi huenda kiwango chake kingeshuka au asipate klabu kubwa ya kuitumikia.

Kipa huyo ameingia katika anga za ushindani mkubwa na ‘Tanzania One’ Aishi Manula ambapo atatakiwa kufanya kazi kubwa zaidi kuhakikisha anamuweka benchi na yeye kupoka nafasi hiyo licha ya uwezo wake mkubwa.

Juma Balinya

Ni ukweli kwamba mabeki wa timu pinzani wanapaswa kujiandaa kisaikolojia juu ya uwezo mzuri wa wa kufunga.

Balinya alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda akimaliza akiwa na mabao 19 na kupokea kiatu chake cha dhahabu.

Uwezo wa mshambuliaji huyo ni wazi umewavutia vigogo wa Jangwani na kuona hapa ndipo mahali sahihi kwa wao kupata huduma ya mchezaji huyo ambaye wengi walidhani huenda angetua Simba kutokana na tetesi nyingi zilizokuwa zikimuhusisha.

Gerson Viera

Huyu ni beki raia wa Brazil ni kipande cha mtu, kupitia video zake chache zinaonyesha ana uwezo mzuri wa kukaba, pia ni mzuri katika kupiga mipira mirefu na kupandisha mashambulizi.

Beki huyo (26), aliwahi kucheza Gremio ya Brazil amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea ATK ya India.

Beki huyo amezua gumzo kwa baadhi ya mashabiki wa soka baada ya taarifa kuwa aliwahi kucheza na baadhi ya nyota duniani akina Neymar, Philippe Coutinho, Casemiro na Alison Beka kipa wa Liverpool akiwa na miaka 17.

Ujio wa kipa huyo unatoa tafsiri kuwa nyota huyo ataleta changamoto mpya kwa wachezaji kama Erasto Nyoni, ambaye ameongeza mkataba, Pascal Wawa na Yusuf Mlipili kama wataendelea kusalia katika kikosi hicho.

Mapinduzi Balama

Ni kiungo fundi akiwa na uwezo wa kukaba. Balama amesajiliwa na Yanga akitokea Alliance kwa mkataba wa miaka mitatu, baada ya kucheza kwa kiwango bora msimu uliopita.

Pengine ni mchezaji ambaye Yanga inategemea mengi zaidi kutokana na ubora wake na ndiyo maana ni mchezaji pekee msimu huu ambaye ametia saini mkataba wa miaka mitatu ndani ya timu hiyo huku wengine wakimwaga wino miwili.

Sharaf Eldin

Kwa muonekana mchezaji huyo raia wa Sudan aliyesajiliwa na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Al-Hilal, anaonekana ni hodari.

Kiungo huyo amewahi pia kuitumika El-Merreikh ya Sudan huenda akawa miongoni mwa viungo warefu zaidi akiwa na urefu wa sentimita 1.8 na umri wa miaka 17.

Kiwango chake bora kiliwahi kumtambulisha katika soka nchini Sudan ambapo amewahi kutamba katika kikosi cha timu ya taifa.

Ujio wake unaleta changamoto kwa baadhi ya wachezaji wa viungo wa Simba akiwemo Jonas Mkude na Clatous Chama ambao wamejihakikishia kubaki baada ya kutia saini mikataba mipya.

Hata hivyo, wachezaji wa kiungo kama Said Ndemla, Mzamiru Yassin wanapaswa kufanya kazi ya ziada kupata namba katika kikosi cha kwanza msimu ujao.

AbdulAziz Makame

Kiungo mwingine fundi ambaye sio mgeni machoni mwa Watanzania wengi, aliwahi kuwa katika kikosi cha vijana cha Simba miaka kadhaa iliyopita ambapo alikuwa na akina Jonas Mkude, Said Ndemla, Ibrahim Ajibu, Peter Manyika na baadaye aliamua kutafuta maisha mengine.

Makame ametia saini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga kwa mashindano ya msimu ujao.

Ni mchezaji miongoni mwa wachache wanapatikana Zanzibar ambaye amebarikiwa kipaji cha aina yake na ndiyo maana ameweza kuwa kivutio Yanga.

Tangu mwaka 2015 alipoanza kuitumikia Mafunzo FC ya Zanzibar, nyota huyo mwenye uwezo wa kupiga pasi ameweza kujitunza na kuonekana bado bora, hivyo ataongeza idadi ya wachezaji kwa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’.

Makame anatarajiwa kucheza kwa kiwango bora Yanga kutokana na uwezo wake uwanjani.

Advertisement