Wapinzani wa Taifa Stars Chan hawa hapa

Wakati mwezi ukielekea ukingoni, habari kubwa yenye mvuto wa kipekee kwa wadau wa mpira wa miguu nchini ni kitendo cha timu yetu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika Kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (Chan).

Ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sudan katika mchezo uliochezwa jijini Khartoum Oktoba 18 ulitosha kuivusha Taifa Stars na kuipeleka kwenye Fainali za Chan 2020 zitakazofanyika Cameroon mwakani, ikinufaika na kanuni ya bao la ugenini licha ya kupoteza kwa bao 1-0 Dar es Salaam, Septemba 22.

Kwa kufuzu huko, Tanzania ni miongoni mwa mataifa 16 yatakayoshiriki mashindano hayo ambayo tarehe ya kufanyika kwake hata makundi kwa timu zinazoshiriki hayajapangwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf). Timu 16 zilizofuzu kila moja imekuwa na historia na kumbukumbu zake katika mashindano ya Chan ambapo kuna ambazo zimewahi kufanya vizuri pindi ziliposhiriki siku za nyuma na pia zipo zilizochemsha.

Kuna mataifa yaliyowahi kushiriki na pia yapo ambayo hayakuwahi kupata fursa ya kuwemo kwenye Chan na hii itakuwa ni mara ya kwanza kushiriki.

Kwa kulitambua hilo, Spoti Mikiki inakuletea dondoo za timu 15 ambazo zitaungana na Taifa Stars katika Chan ili kuwapa wasomaji, wadau na mashabiki wa soka nchini, taswira halisi ya nini timu hiyo inakwenda kukutana nacho katika mashindano hayo.

Burkina Faso

Imefuzu Fainali za Chan ikiwa moja ya timu tano kutoka kanda yenye nchi zinazounda Muungano wa Vyama vya Soka Afrika Magharibi (Wafu) ambapo ilitinga kwenye mashindano hayo kwa kuiondosha Ghana kwa ushindi wa bao 1-0 katika mechi mbili za raundi ya pili ambapo ilishinda nyumbani kabla kulazimisha suluhu ugenini.

Burkina Faso inayonolewa na kocha mzawa Kamou Malo mwenye umri wa miaka 56, itakuwa ni mara ya tatu kushiriki Fainali za Chan ambapo imewahi kufanya hivyo mwaka 2014 na 2018 na mara zote imeishia hatua ya makundi.

Cameroon

Itashiriki Fainali za Chan kwa tiketi ya uenyeji na hapana shaka kocha Toni Conceicao raia wa Ureno mwenye miaka 57 ndiye ataongoza harakati za timu hiyo kubakiza ubingwa nyumbani.

Mafanikio makubwa katika mashindano hayo ni kutinga robo fainali wakifanya hivyo mara mbili tofauti waliposhiriki mwaka 2011 na 2016 huku wakiishia hatua ya makundi mwaka 2018 na hii itakuwa mara ya nne kwao kushiriki.

Congo

Ni moja ya timu ambazo zimeonja ladha ya kushiriki mashindano hayo ambapo awamu hii takuwa ni mara ya tatu kwao. Mwaka 2014 walipoishia hatua ya makundi na mwaka 2018 robo fainali.

Wamefuzu kutoka kanda inayojumuisha nchi zinazounda Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika ya Kati (UNIFFAC) na timu itakuwa chini ya kocha Valdo Filho raia wa Brazil mwenye miaka 55.

DR Congo

Inaingia kwenye fainali hizo ikiwa ni timu iliyofanikiwa kuliko nyingine ambapo imetwaa ubingwa mara mbili mwaka 2009 na 2016. Pia ilifika robo fainali mara mbili 2011 na 2014.

Kundi kubwa la wachezaji wake wanatoka TP Mazembe na AS Vita ambazo zimekuwa zikifanya vyema kwenye mashindano ya Afrika na si jambo la ajabu kuona ni miongoni mwa timu zilizoshiriki fainali hizo mara nyingi kwani hii itakuwa ni mara ya tano, wakikosa fainali za awamu iliyopita tu.

Guinea

Ushiriki wa mara kwa mara wa klabu mbili kubwa Horoya na Hafia katika mashindano ya klabu Afrika, umekuwa chachu kwa Guinea kuwa miongoni mwa timu zinazopata fursa ya kushiriki Chan katika miaka ya hivi karibuni.

Tangu iliposhiriki mara ya kwanza mwaka 2016 nchini Rwanda na kufika robo fainali, Guinea ilishiriki tena mwaka 2018 na hii itakuwa ni mara ya tatu mfululizo kwao ingawa hawajawahi kupata mafanikio makubwa.

Mali

Ni miongoni mwa mataifa tishio zinapofika Fainali za Afrika (Afcon) na zile za kuwania kufuzu Kombe la Dunia lakini haijaweza kuhamisha makali yao kwenye mashindano ya Chan ingawa imekuwa ikishiriki mara kadhaa. Hii ni mara yao ya nne kushiriki fainali hizo. Mali imewahi kutinga hatua ya robo fainali mwaka 2014.

Morocco

Inaingia kama moja ya mataifa inayopewa nafasi ya kutwaa ubingwa kutokana na kikosi chake kuundwa na kundi kubwa la wachezaji bora na vipaji wakitokea klabu za Raja Casablanca, Wydad Casablanca, RS Berkane na Hassania Agadir.

Ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo wakiwa wametwaa taji hilo mara moja mwaka 2018 pindi fainali hizo zilipofanyika nchini mwao na hii itakuwa ni mara ya nne kushiriki Chan.

Namibia

Haionekani kama timu tishio lakini mara moja iliyoshiriki mwaka 2018, ilishtua wengi kwa kufuzu hatua ya robo fainali waliyochapwa mabao 2-0 na Morocco.

Kocha mzawa Ricardo Mannetti mwenye miaka 44 ndiye aliyekiongoza kikosi hicho kutinga Fainali za Chan kupitia tiketi ya nchi zinazounda Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) baada ya kuzitupa nje Comoro na Madagascar.

Niger

Ni mara ya tatu kushiriki Fainali za Chan wakiwa tayari wameshafanya hivyo mwaka 2011 katika fainali zilizofanyika Sudan huku pia nyingine ikiwa ni katika mashindano yaliyoandaliwa Rwanda mwaka 2016. Mafanikio yao makubwa ni kutinga hatua ya robo fainali katika Fainali za mwaka 2011.

Rwanda

Ndio taifa la Afrika Mashariki lenye mafanikio kwenye mashindano hayo na hayo ni kutinga hatua ya robo fainali wakifanya hivyo mwaka 2016 walipokuwa wenyeji. Hii ni mara ya nne kushiriki iliwahi kushiriki mwaka 2011 na 2018 ambapo iliishia hatua ya makundi.

Kikosi kinaundwa na kundi kubwa la wachezaji wa APR, Rayon Sports na AS Kigali kinaongozwa na kocha mzawa Vincent Mashami.

Togo

Taifa hilo la Afrika Magharibi litaenda Cameroon likiwa linashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo ya Chan kwani hapo awali halijawahi kupata nafasi ya kucheza fainali hizo katika awamu tano zilizopita.

Haikuwa kazi rahisi kwao kujihakikishia tiketi ya kwenda Cameroon na walilazimika kuzitoa timu za Benin na Nigeria katika mashindano ya kuwania kufuzu.

Tunisia

Wameshawahi kuonja ladha ya ubingwa wa mashindano hayo wakifanya hivyo mara moja katika fainali zilizofanyika Sudan ambako waliibuka vinara baada ya kuichapa Angola kwa mabao 3-0 katika mchezo wa fainali. Kocha mzawa Mondher Kebaier atakuwa anawategemea zaidi nyota wa CS Sfaxien, Esperance na Etoile Du Sahel kusaka taji la pili la mashindano hayo ambayo wanashiriki kwa mara ya tatu, mara moja wakifika robo fainali mwaka 2016.

Uganda

Wamefuzu fainali hizo wakiwa chini ya kocha mzawa Abdallah Mubiru ambaye haijajulikana kama atapewa fursa ya kuendelea au jukumu hilo litabebwa na kocha mkuu wa jumla wa timu ya taifa Jonathan McKinstry.

Uganda sio tishio kwenye mashindano hayo, ni timu yenye uzoefu wa kutosha kwani imeshiriki fainali hizo mara nne mfululizo kuanzia ile ya mwaka 2011 iliposhiriki mara ya kwanza hadi zile za mwaka jana nchini Morocco. Hii ni mara ya tano kushiriki na watawategemea zaidi nyota wa klabu za KCCA, Proline, Vipers na URA.

Zambia

Timu hiyo imefuzu kupitia tiketi ya Cosafa na hii itakuwa ni mara ya nne kwao kushiriki mashindano hayo ikiongozwa na kocha mzawa na nyota wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Aggrey Chiyangi mwenye miaka 55.

Mafanikio ya Zambia katika mashindano hayo ni kumaliza nafasi ya tatu mwaka 2009 na mara mbili nyingine ilizoshiriki 2016 na 2018 ikiishia hatua ya robo fainali

Zimbabwe

Hii itakuwa ni mara ya nne kwao kushiriki huku mafanikio makubwa kwao yakiwa ni kumaliza kwenye nafasi ya nne mwaka 2014 zilipofanyika nchini Afrika Kusini na mara nyingine tatu ikiishia hatua ya makundi.