Mambo 5 Maalim Seif anatakiwa kuyafanya ili kumnusuru kisiasa

Dar es Salaam. Wakati Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikimtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), upande wa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif umezidi kuwa katika wakati mgumu zaidi baada ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kuisajili bodi ya wadhamini ya chama hicho iliyopendekezwa na upande wa Profesa Lipumba.

Kutambuliwa kwa Profesa Lipumba na taasisi hizo nyeti kunatengeneza mazingira magumu ya kisiasa kwa upande wa Maalim Seif, jambo ambalo linamsukuma kufanya moja kati ya mambo matano ili aendelee kuwapo kwenye siasa hai kama alivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.

Chama hicho kimedumu kwenye mgogoro wa ndani tangu Agosti, 2015 baada ya Profesa Lipumba kutangaza kujiuzulu uenyekiti ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Juni 13, 2016, Profesa Lipumba alitangaza kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu na licha ya mkutano mkuu wa CUF kuikubali barua yake ya kujiuzulu, alirejea kwenye nafasi yake, jambo lililosababisha mgogoro ndani ya chama hicho.

Mgogoro huo uliongezeka zaidi baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuweka wazi kwamba anamtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho licha ya kuwapo kwa mgogoro huo.

Hali iliendelea kuwa mbaya zaidi baada ya pande hizo kugawana majengo ya ofisi, upande wa Profesa Lipumba ukishikilia zilizopo Tanzania Bara wakati upande wa Maalim Seif ukishikilia ofisi za Zanzibar.

Juni 4, wabunge 40 wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif walifungua ofisi yao ya wabunge jijini Dar es Salaam na kutenga chumba kimoja kwa ajili ya kiongozi huyo ili aweze kutekeleza majukumu yake akiwa Tanzania Bara.

Ilipofika Juni 12, Rita iliisajili bodi ya wadhamini ya CUF upande wa Profesa Lipumba. Rita ilisema ilifanya mawasiliano na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kabla ya kuchukua uamuzi huo.

 Kitendo hicho kinazidi kuupa nguvu na uhalali  upande wa mwenyekiti huyo ambaye alipojiuzulu alitoa sababu ya ‘dhamira kumsuta’ kutokana na vyama vinavyoundwa na Ukawa kumpokea Edward Lowassa kuwa mgombea urais.

Kuhusu suala la ruzuku, upande wa Maalim Seif ulilalamika kwamba upande wa Profesa Lipumba unapokea ruzuku ya chama wakati siyo uongozi unaotambulika. Suala hilo liliwasukuma kufungua shauri mahakamani kutaka ruzuku ambayo ulipokea kabla ya kusitishwa irudishwe.

Kwa ujumla inaonekana, mazingira hayo ya kisiasa yameubana upande wa Maalim Seif kiasi cha kulazimika kufanya jambo moja kati ya haya matano; kwanza ni kufanya suluhu na Profesa Lipumba ili wafanye kazi pamoja na kuunganisha makundi yao.

Licha ya kwamba Maalim Seif ameweka msimamo mkali kwamba hayupo tayari kukaa meza moja na Profesa Lipumba kwa sababu hatambuliki, mwenyekiti huyo amesema yupo tayari wakati wowote kukaa na katibu huyo wa CUF  kuzungumza na kumaliza tofauti zao.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kiasisa wamesema Maalim Seif akitaka kupata urahisi wa kufanya siasa, akubali kuzungumza na mshirika wake huyo wa zamani ambaye anatambulika na taasisi zinazosimamia vyama vya siasa nchini.

Jambo jingine linaloweza kumweka Maalim Seif salama kisiasa ni kuhamia chama kingine cha siasa. Katiba ya Jamhuri ya Muungano inabainisha kwamba mtu yeyote ana haki ya kuhama chama na kuhamia katika chama kingine.

Pengine jambo hilo linaweza kuwa gumu kwa Maalim Seif, lakini ni njia rahisi pia ya kumfanya akaendeleze harakati zake za kisiasa kwenye chama ambacho hakina mpasuko kama ilivyo kwa chama chake ambako taasisi za Serikali inaonekana kuutambua upande wa Profesa Lipumba.

Maalim Seif anaweza pia kuanzisha chama kingine cha siasa ili aachane na CUF jambo ambalo ni gumu na hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho.

Jambo jingine ambalo Maalim Seif anaweza kulifanya ni kwenda mahakamani dhidi ya ofisi ya Vyama vya Siasa na Rita. Tayari upande wa Maalim Seif umefungua kesi kupinga hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa CUF.

Jambo jingine ambalo Maalim Seif anaweza kufanya ni kuachana na siasa ili apate muda wa kupumzika na kufanya mambo mengine. Anaweza kustaafu masuala ya siasa na kubaki kuwa mshauri tu.

Kwa kuzingatia umri wake na mchango wake mkubwa katika siasa za vyama vingi hapa nchini, siyo jambo la kushangaza kuona Maalim Seif akiamua kustaafu siasa na kuamua kujielekeza katika mambo mengine ya kijamii.

Akitoa ushauri wake kwa Maalim Seif, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema mwanasiasa huyo anapaswa kutafuta njia ya kuzungumza na mwenzake (Profesa Lipumba) ambaye tayari ameonyesha utayari wa mazungumzo.

Dk Bana alisema viongozi hao wawili wana nguvu ndani ya chama, hivyo ni jambo la busara wakikutana kuzungumzia tofauti zao na kuendelea kufanya kazi pamoja ili kukijenga chama chao ambacho kina nguvu hasa upande wa Zanzibar.

“Namshauri atafute dirisha la kukutana na mwenzake ili wamalize tofauti zao. Ninaamini wakifanya hivyo, CUF mpya itazaliwa na wataweza kukiimarisha chama chao tofauti na ilivyo sasa,” alisema Dk Bana.

Mbali na ushauri huo, Dk Bana alisema Maalim Seif anaweza pia kuendelea kutafuta haki mahakamani kupitia kesi aliyoifungua ili haki itendeke.

Lakini, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) alisema kitu anachokiona ni Maalim Seif kwenda kuanzisha chama chake cha siasa ambacho kitatoa ushindani mkubwa kwa CUF.

“Unajua Maalim Seif ana mtaji mkubwa wa wafuasi, kwa hiyo akiamua kuondoka CUF na kuanzisha chama chake atapata nguvu kubwa na chama hicho kitatoa ushindani kwa CCM na CUF yenyewe,” alisema Profesa Mpangala.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), John Samba alisema mpasuko ndani ya CUF ndiyo utakaomfanya Maalim Seif kuachana na siasa kwa sababu anakosa nguvu kutoka kwenye taasisi za umma.

Samba alisema siasa za Tanzania ni ngumu kwa sababu hakuna mazingira sawa na kila chama cha siasa kinaangalia masilahi yake hata kama vitashirikiana.

Pia, alisisitiza kuwa jambo mgogoro uliopo ndani ya CUF umempunguzia nguvu Maalim Seif katika siasa zake baada ya uchaguzi wa mwaka 2015.

“Maalim Seif amekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu, nadhani ni wakati aachane na siasa. Sasa hivi naona mambo yamekuwa magumu kwake kwa sababu upande mwingine (wa Lipumba) unapata legitimacy (uhalali) kuliko upande wake,” alisema.