Wahariri kujadili mabadiliko ya tabianchi

Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Nevile Meena

Muktasari:

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) linakutana jijini Dodoma kwa siku mbili, litajadili pia uchaguzi ujao nchini

Dodoma. Wahariri nchini wanakutana jijini Dodoma kujadili masuala yanayohusu nchi na ustawi wa vyombo vya habari, mada kuu ikiwa nafasi ya vyombo hivyo katika matumizi ya gesi asilia kwa ajili ya kulinda misitu.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Aprili 28, 2024 na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mkutano mkuu wa 13 wa kitaaluma wa jukwaa hilo.

Amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko. Pia atakuwapo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Amesema hivi sasa Tanzania inapitia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, yakiwamo mafuriko ambayo yametokea maeneo kadhaa ya nchi kwa sababu ya mvua kubwa iliyonyesha.

Meena amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuwahabarisha Watanzania kuhusu madhara ya kuharibu mazingira kwa sababu mabadiliko ya tabianchi yanayoonekana sasa yamesababishwa na uharibifu wa mazingira kwa kukata misitu hovyo.

“Kuna watu ambao wanaharibu misitu na wengine kufanya shughuli za kilimo kwenye vyanzo vya maji, hawa wasipodhibitiwa ndiyo wanakuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira unaosababisha watu kukosa maji,” amesema.

Meena amesema mada zingine zitakazojadiliwa ni nafasi ya mwanamke katika vyumba vya habari, haki zao wajibu wao pamoja na uzingatiaji wa taaluma.

Pia, mada kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, matumizi ya akili bandia kwenye vyumba vya habari na matumizi ya kidijitali.

“Kama mnavyojua mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani tukijaliwa tutakuwa na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, Rais wa Zanzibar na Baraza la Wawakilishi, hivyo sisi kama vyombo vya habari tunajipanga kuhakikisha tunaripoti habari ambazo zitalivusha salama Taifa kwenye uchaguzi huo,” amesema Meena.

Mwandishi mkongwe ambaye pia ni mjumbe wa kamati tendaji ya TEF, Salim Mohamed Salim amewataka waandishi wa habari kuchagua habari za kuandika kwenye uchaguzi mkuu na kuachana na taarifa ambazo zitazua taharuki na kuleta machafuko nchini.

Amesema wagombea wote watakaotumia lugha za kejeli, kashfa na matusi wasipate nafasi kwenye vyombo vya habari kwa sababu kama watapewa, madhara yake yatakuwa ni makubwa kwani yanaweza kuleta machafuko nchini.

Mkutano huo utakaowakutanisha wahariri 150 utafanyika kesho Aprili 29 hadi 30, 2024.