Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahariri kujifungia kujadili mchakato mabadiliko ya Sheria ya Habari

Muktasari:

  • Mawaziri wawili wanatarajiwa kuhudhuria Kongamano la Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) litakalofanyika Morogoro, mawaziri hao ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro.

Dar es Salaam. Wahariri wa vyombo vya habari nchini kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) wanatarajia kujadili pamoja na mambo mengine, mchakato wa mabadiliko ya Sheria za Huduma za Habari ya mwaka 2016 katika kongamano la siku nne litakalofanyika Morogoro.

 Mgeni rasmi katika kongamano hilo la 12 la TEF anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na litafanyika kuanzia Machi 29 hadi Aprili 2, 2023 mjini Morogoro.

Februari 10, 2023, muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali ulio na mapendekezo ya sheria nane ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari, uliwasilishwa bungeni ikiwa ni hatua ya pili baada ya wadau kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko hayo.

Baada ya muswada huo kusomwa bungeni kwa mara ya kwanza, sasa umepelekwa kwenye kamati ya bunge na wadau watapata fursa ya kutoa maoni zaidi ili kuiboresha sheria hiyo inayosimamia sekta ya habari.

Akizungumzia kongamano hilo, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF, Neville Meena amesema mbali na Nape, pia jukwaa hilo linategemea kuwepo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro.

“Kongamano hili huwa tunafanya kila mwaka kwenye mikoa mbalimbali, safari hii tumeamua kufanyia hapa Morogoro,” amesema Meena.

Kwenye kongamano hilo, Meena amesema kutakuwa na mada sita ambazo ni kuangalia utendaji wa vyombo vya habari, taaluma na maadili na wanawake katika habari na hatari ya kutoweka kwao kwenye vyumba vya habari.

Mada zingine amesema ni uchumi wa vyombo vya habari na jinsi ya kuvinusuru; mabadiliko ya teknolojia, ukuaji na ujenzi wa mitandao ya kijamii yenye viwango vya kitaaluma na mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari na mweleko wake.

Meena amesema mada ya mwisho itakuwa ni vyombo vya habari na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Uchaguzi sio tukio, ni mchakato. Inahitajika kuandaa watu na kuwashawishi kushiriki kwenye uchaguzi, vyombo vya habari vinawekeza fedha kwenye uchaguzi huo, hivyo ni sehemu muhimu kwenye kongamano hili,” amesema.

Kwa upande wake, Jane Mihanji ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Tef, amesema, miongoni mwa sababu kuweka mada inayohusu wanawake na vyombo vya habari ni kutokana na tafiti kuonesha kwamba kuna unyanyasaji wa wanawake kwenye vyombo vya habari.

“Tumekuwa tukihimiza kuwa na ushiriki sawa. Baadhi ya tafiti zinaonesha wanawake wanaopewa nafasi za juu ni wachache. Tafiti za Tamwa, Internews na zingine zinaonesha kuwa kumekuwa na unyanyasaji wa wanawake kwenye vyumba vya habari.

“Taarifa zao zimekuwa hazitoki, hivyo wamekuwa wakikimbia vyumba vya habari,” amesema Jane.