VIDEO: Mbowe abainisha ugonjwa uliomlaza Muhimbili

Muktasari:

Mbowe alianguka ghafla usiku wa kuamkia juzi, nyumbani kwake Mikocheni.


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameruhusiwa kutoka hospitali alikokuwa akitibiwa na kueleza kuwa kilichokuwa kikimsumbua ni msongo wa mawazo na uchovu kupita kiasi.

Mbowe alianguka ghafla usiku wa kuamkia juzi, nyumbani kwake Mikocheni.

Akizungumza na Mcl digital akiwa wodini, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mbowe amesema afya yake inaendelea vyema kwa sasa.

Kuhusu  ugonjwa wake Mbowe amesema umesababishwa na msongo wa mawazo na uchovu kutokana na kufanya kazi usiku na mchana.

"Juzi nilitoka Dodoma kwanza ilikuwa nakuja kwa ajili ya kesi inayotukabili viongozi wa Chadema,  nikiwa njiani nikapata taarifa za msiba wa kaka yangu ambao kimsingi upo nyumbani kwangu, "amesema

“Ukiacha hayo kwa muda mrefu tumefanya kazi bila kupumzika, tulikuwa tunatayarisha hotuba ya kambi rasmi ya upinzani kazi ambayo imechukua muda mwingi,"amesema

Amesema alipokelewa vizuri MNH na kupata huduma bora kutoka kwa madaktari wake.

"Leo nimeruhusiwa narudi nyumbani baada ya msiba nitaendelea na vipimo vingine ambavyo nitaangalia nifanyie ndani au nje ya nchi kulingana na madaktari wangu watakavyoona,"amesema