Mbunge ahoji mkakati wa Serikali kukomesha vifo vya mahabusu mikononi mwa polisi

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya ndani, Kangi Lugola amesema kifo ni mtego na hakichagui sehemu ya kutokea.

Dodoma. Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) ameihoji Serikali kuhusu mkakati yake katika kukomesha matukio ya mahabusu wanaodaiwa kufia mikononi mwa polisi.
"Mheshimiwa Spika, ni aibu, fedheha na huzuni kuona mahabusu wakifia mikononi mwa polisi wakiwa mahabusu, je Serikali inasema nini kuhusu jambo hili," amehoji Khatib leo Septemba 13 akiwa bungeni.
Akijibu  swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema suala la mtu kufa halichagui mahali anapotakiwa kufia kwani kifo ni mtego.
Waziri Lugola ametumia kitabu cha Biblia katika Mhubiri 9 akinukuu kuwa kifo ni mtego na kila mtu amewekewa.
"Wengine wanaweza kufia kwenye magari, bungeni na hata wengine wanakufa wakifanya mapenzi, je huko nako kuna nini," amesema Lugola.
Waziri amewataka wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi kwa kuchoma vituo vya polisi inapotokea mtuhumiwa kafia kituoni kwani kama watafanya hivyo mbona hawachomi vitanda na nyumba wanazofia watu wakijamiiana?