Nasri naye amtetea kocha Wenger

Muktasari:

Wenger amekuwa katika wakati mgumu kutokana na kuwa na matokeo mabaya katika siku za karibuni.

Arsene Wenger ametetewa na mmoja wa nyota wake wa zamani, Samir Nasri baada ya kumzungumzia kocha wake huyo wa zamani.

Wenger amekuwa katika wakati mgumu kutokana na kuwa na matokeo mabaya katika siku za karibuni.

Lakini Nasri, mmoja kati ya nyota waliosajiliwa na Wenger kwa mafanikio, anaamini wachezaji wa sasa wanacheza chini ya kiwango.

"Huwezi kumlamu mtu kama Wenger, hilo haliwezekani," alisema Nasri alipozungumza na Sky Sports.

"Arsenal ni klabu kubwa lakini yeye pia amechangia kuifanya klabu hiyo kuwa kubwa zaidi.

"Ninadhani watu wanatakiwa kuwa na usawa, si tatizo lake kwa Arsenal kuwa hivi. Ni wachezaji uwanjani ambao wanasababisha matokeo.

"Kuna mambo yametokea ndani ya Arsenal, ndani ya bodi, kwa wachezaji maeneo yote yanatakiwa kuangaliwa, lakini si kumwangalia Arsene pekee."

Nasri alikuwa mmoja kati ya wachezaji maarufu katika klabu hiyo ya Kaskazini mwa London, kabla ya kuikana Arsenal ya Wenger na kujiunga na Manchester City 2011.