Zanaco yamrudisha Lwandamina Zambia
Muktasari:
- Yanga na Zanaco zitacheza siku 19 zijazo, kati ya Machi 11 na 13, mchezo wa kwanza wa mzunguko wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
- Lwandamina, kabla ya kujiunga na Yanga, alikuwa akiifundisha Zesco inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia.
Dar es Salaam. Bao lililofungwa na Taonga Bwembya wa Zanaco ya Zambia dhidi ya APR ya Rwanda katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mjini Kigali, limeifanya timu hiyo kumrudisha kwa muda kocha wa Yanga, George Lwandamina nchini Zambia, wakati timu hiyo itakapocheza na mabingwa hao wa Tanzania, mchezo wa raundi ya kwanza wa ligi hiyo.
Yanga na Zanaco zitacheza siku 19 zijazo, kati ya Machi 11 na 13, mchezo wa kwanza wa mzunguko wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Lwandamina, kabla ya kujiunga na Yanga, alikuwa akiifundisha Zesco inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia.
Timu hizo zimefuzu baada ya kushinda michezo yao, Yanga iliitoa Ngaya ya Comoro kwa jumla ya mabao 6-2, mchezo wa kwanza, Yanga iliifumua timu hiyo mabao 5-1 kabla ya kutoka sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam jana.
Mchezo wa kwanza wa Zanaco na APR mjini Lusaka, timu hizo zilitoka suluhu lakini jana, kocha wa Zanaco, Mumamba Numba aliondoka Uwanja wa Amahoro kwa kicheko baada ya timu yake kushinda bao 1-0 lililofungwa na Bwembya dakika ya 17.
Yanga ilikutana na Zanaco 2006 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mchezo wa kwanza, mabingwa wa Tanzania waliifunga Zanaco 2 -1 na marudiano, Yanga ililala kwa mabao 2-0 na kuondoshwa kwenye mashindano hayo. Mchezaji pekee wa Yanga aliyecheza mechi hiyo, ambaye bado yupo kwenye kikosi cha Yanga ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Yanga vs Ngaya
Mchezo wa jana, Yanga ilionekana kutoupa uzito kutokana na hazina ya mabao na kuifanya Ngaya De Mbe ionekane ikicheza kwa kasi na hata kuiweka Yanga kwenye wakati mgumu.
Hali hiyo ilifanya hisia za nyota wa Yanga kuhisi kuwa kuna vitu vya kishirikina katika lango la wapinzani wao na kila mara kuchimba katika nguzo za goli lao.
Ngaya ilianza kwa kulisakama lango la Yanga ndani ya dakika sita za kwanza, lakini umakini mdogo wa washambuliaji wake na uimara wa kipa, Deo Munishi ‘Dida’ ulisababisha timu hiyo kushindwa kufungwa.
Kitendo cha kukosa mabao wakati wanamiliki mpira kiliwafanya nyota wa Yanga kuonekana kama waliohamaki na kujikuta ikishambuliwa kwa kushitukiza.
Ngaya walitumia nafasi ya kupanda kwa Yanga na kufanya shambulizi la kushitukiza, kitu kilichowalipa dakika ya 20, baada ya beki Vincent Bossou kujifunga akiwa katika jitihada za kuokoa mpira wa krosi ya Chadhuil Mradabi.
Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya mashabiki wa Yanga waliojitokeza uwanjani hapo kupiga makofi kana kwamba kilichotokea ni bahati mbaya na wana uhakika wa kuibuka na ushindi.
Yanga waliamua kushambulia mfululizo bila kutumia nafasi walizopata kutokana na umakini wa mabeki wa Ngaya, ambao walionekana kutulia zaidi huku wakishambulia kwa kushitukiza.
Wachezaji wa Yanga walianza kujaribu mashuti ya mbali na juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 43, wakati Mwinyi Haji alipoisawazishia Yanga kwa mkwaju wa mita 30 na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko kwa sare ya bao 1-1.
Yanga ilionekana kurudi kwa kasi kipindi cha pili, lakini umakini mdogo wa Obrey Chirwa ulishindwa kuipa bao la pili timu yake dakika ya 52.
Wawakilishi wengine wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho, KVZ ya Zanzibar wameshindwa kutamba baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Messenger Ngozi nchini Burundi.
Timu hiyo imetolewa kwa jumla ya mabao 4-2, kwani mchezo wa kwanza, KVZ ilishinda mabao 2-1. Zimamoto iliyoifunga Ferroviario de Maputo mabao 2-1 mchezo wa kwanza, itashuka uwanjani leo mjini Maputo, Msumbiji kwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga ibadilike
Licha ya kufuzu kwa kwa hatua ya kwanza, Yanga itahitaji kubadilika zaidi kama itahitaji kusonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Eneo la ushambuliaji linahitai kuongeza umakini kutokana na kile walichokionyesha mechi ya jana.