Miili ya mashujaa waliouawa yaletwa, aliyepotea apatikana

MAPOKEZI YA MIILI 14 YA WANAJESHI WALIOFARIKI KONDO DRC

Muktasari:

Hata hivyo, Jenerali Mabeyo alisema jeshi hilo linachukua kila tahadhari kuhakikisha tukio kama hilo halijirudii tena.

Dar es Salaam. Askari mmoja kati ya wawili waliokuwa wamepotea baada ya kushambuliwa na kikundi cha waasi ADF nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC), amepatikana huku majeruhi wakitawanywa kwa kupelekwa Kinshasa nchini humo na wengine Uganda kwa matibabu zaidi.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo baada ya kupokea miili 14 ya wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakilinda amani DRC na kuuawa na ADF Desemba 7. Katika shambulio hilo, wanajeshi 44 walijeruhiwa baadhi hali zao zikielezwa ni mbaya. Miili hiyo ilipokelewa uwanja wa ndege wa JWTZ Ukonga.

“Taarifa tulizopewa mpaka sasa ni kwamba majeruhi 44 wote wanaendelea vizuri. Kwa ambao hali zao ni mbaya wamepelekwa Kinshasa (DRC) na wengine nchini Uganda kwa matibabu zaidi,” alisema Jenerali Mabeyo na kuongeza: “Kati ya wale wawili waliokuwa wamepotea mmoja tayari amepatikana, amebaki mmoja ambaye hajapatikana.”

Hata hivyo, Jenerali Mabeyo alisema jeshi hilo linachukua kila tahadhari kuhakikisha tukio kama hilo halijirudii tena. “Wale waasi wao wanapigana lakini sisi tunalinda amani. Unapolinda amani lazima utegemee lolote na unaposhambuliwa unaangalia wapi umekosea, unajisahihisha, hatuna hofu tutaendelea kulinda amani na si DRC pekee na kwingineko,” alisema.

Naye waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi alitoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao huku akisema kila juhudi zitachukuliwa ili jambo hilo lisijirudie.

“Hili ni tukio la kawaida kutokea katika ‘Mission opereshion’ kila juhudi zinachukuliwa ili isijirudie tena,” alisema Dk Mwinyi na kuongeza kuwa JWTZ liko imara.