Mke wa bilionea Msuya aomba kuonana na Rais Magufuli

Muktasari:

Asema katika kesi inayomkabili kuna jambo limejificha kwa kuwa upelelezi haujakamilika katika kipindi cha miaka miwili


Dar es Salaam. Miriam Mrita mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya mdogo wa mumewe, bilionea Erasto Msuya ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu impe nafasi ya kuonana na Rais John Magufuli kwa madai kuwa hatendewi haki katika kesi yake.

"Nimesimama hapa mahakamani naona kuna hila inaendelea nyuma ya kesi hii na sitendwi haki naomba kuonana na rais au makamu wa rais, nieleze matatizo yangu,” amesema Miriam leo Juni 25, 2018 mahakamani hapo jijini Dar es Salaam. Miriam anatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya Aneth Msuya ambaye ni mdogo wake bilionea Msuya ambaye pia ni marehemu.

Ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita kuieleza mahakama kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na jalada la kesi hiyo limeshatoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), sasa limerudishwa kwa wakili anayelishughulikia kwa ajili ya kukamilisha maelekezo aliyopewa.

Baada ya Mwita kueleza hayo, Miriam alinyanyua mkono akiashiria kutaka apewe nafasi na hakimu ili aweze kuzungumza.

“Ni mwaka wa pili sasa nipo mahabusu na upelelezi dhidi ya kesi yangu ya mauaji bado haujakamilika na Juni 4, mwaka huu niliomba uindwe tume huru kuchunguza kesi hii,” amesema.

" Kutokana na hali hii naiomba mahakama inipe nafasi niweze kuonana na Rais John Magufuli au makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanamke mwenzangu ili niweze kueleza matatizo niliyonayo, kwa sababu naona sitendewi haki katika kesi yangu.”

Amesema ni mjane anaona haki yake ya msingi inacheleweshwa katika kesi hiyo, hivyo yupo tayari kuongea sehemu yoyote, endapo atapewa nafasi.

Alipoulizwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba kuwa kesi yake inacheleweshwa na nani, amesema inacheleweshwa na mahakama kwa kuwa upelelezi unacheleweshwa na kwamba kuna jambo limejificha nyuma ya kesi hiyo.

 

Hata hivyo, wakili Mwita amesema mahakama haina mamlaka yoyote ya kuunda tume ya kuchunguza malalamiko yaliyowasilishwa na mshtakiwa.

"Kuna njia nyingi za kuwasiliza malalamiko haya, kama kuandika barua na kumkabidhi wakili wake ambaye naye ataiwasilisha kwa mkuu wa gereza husika,” amesema wakili Mwita.

Hakimu Simba akijibu hoja hizo mbili amesema jukumu la mahakama hiyo ni kuhakikisha upelelezi wa kesi unakamilika ili hatua nyingine ziweze kufuatwa, hivyo kama mshtakiwa ana malalamiko anapaswa kuyawasilisha kwa barua kupitia wakili wake.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 9, 2018 na kuutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa wanakamilisha maelekezo waliyopewa na DPP kwa wakati ili kesi hiyo iweze kuendelea na hatua nyingine.