Idadi ndogo ya wapiga kura wajitokeza asubuhi Mhandu, Senga

Muktasari:

Kujitokeza kwa watu kidogo kwasababishwa na mvua, ibada

Geita/Mwanza. Mvua kubwa inayonyesha tangu alfajiri pamoja na watu wengi kuwahi ibadani nyakati za asubuhi jijini Mwanza imesababisha watu wachache kujitokeza tangu vituo vya kupigia kura katika kata ya Mhandu vilipofunguliwa saa 12:00 alfajiri.

Kutokana na hali hiyo wasimamizi wa uchaguzi wapo katika vituo vya kata hiyo wakisubiri wapiga kura.

 Katika Kata za Senga wilayani Geita pia upigaji kura umeanza kwa kusuasua tangu saa 12:00 kutokana na idadi ndogo ya wananchi kujitokeza.

 Msimamizi Msaidizi wa kituo cha kupiga kura  katika kituo cha Muungano D kilichopo Shule ya Msingi Senga, Maluja Mabomboka amesema taratibu zote zimekamilika wanasubiri tu wapiga kura watakaofika kutimiza haki yao ya kikatiba ya kumchagua diwani wao.

"Wananchi wachache wameanza kujitokeza tangu saa 1:00 asubuhi, mwitikio siyo mzuri kama tulivyotarajia. Labda idadi itaongezeka kadri muda unavyoongezeka," amesema Mabomboka.