George Weah ashinda urais Liberia

Muktasari:

Weah alishiriki uchaguzi wa mwaka 2006 na kuagushwa na Ellen Johnson-Sirleaf.

Monrovia. Mwanasoka wa zamani na mshindi wa Tuzo ya Ballon d’Or 1995, George Weah, amechaguliwa kuwa Rais wa Liberia baada ya kukusanya zaidi ya asilimia 60 ya kura zote za uchaguzi wa marudio.

Ushindi wake ulitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Liberia jana Alhamisi, ikisema baada ya asilimia 98.1 ya kura zote kuhesabiwa, mwanasoka huyo bora wa zamani wa dunia alinyakua asilimia 61.5 ya kura zote zilizopigwa Jumanne ya Desemba 26,2017.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Weah  amewashukuru wote waliompigia kura na ambao hawakumpigia.

Weah, mwanasoka wa kwanza wa Afrika kutwaa taji la Mwanasoka Bora wa Mwaka ya Fifa na tuzo ya Ballon d'Or, amewahi kuchezea klabu za AC Milan, Monaco, PSG na Manchester City.

Katika uchaguzi huo, Weah amemshinda aliyekuwa Makamu wa Rais, Joseph Boakai aliyedumu katika wadhifa huo kwa miaka 12.

Weah ameshinda uchaguzi huo wa duru ya pili uliokuwa na ushindani mkali.

Katika uchaguzi huo, Rais Ellen Johnson-Sirleaf ambaye ni rais wa sasa hakugombea kutokana na matakwa ya Katiba ya nchi hiyo ambayo inamzuia kugombea kiti hicho zaidi ya vipindi viwili.

Weah katika uchaguzi wa mwaka 2006 uliompa ushindi Ellen aligombea.