VIDEO: Mzee Majuto kuagwa viwanja vya Karimjee leo

Msanii wa vichekesho Amri Athumani ' King Majuto'

Muktasari:

Amri Athuman’ King Majuto’ alizaliwa 1948 jijini Tanga na kusoma shule Msambweni, Tanga, alianza kuigiza 1958 akiwa na umri wa miaka tisa akiigiza katika majukwaa.

 


Dar es Salaam. Mwili wa msanii wa vichekesho Amri Athumani ' King Majuto' aliyefariki jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, utaagwa leo Agosti 9, 2018 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Rais wa shirikisho la filamu Tanzania , Simon Mwakifamba amesema, Mzee Majuto ataagwa kuanzia saa 8.00 mchana katika viwanja hivyo na saa 10.00 jioni atasafirishwa kwenda nyumbani kwake Tanga kwa mazishi.

“Taarifa ambayo tumewasiliana na familia ni kwamba, Mzee Majuto ndugu jamaa na marafiki watatoa heshima za mwisho na baada ya hapo mwili utaelpelekwa nyumbani kwake Tanga kwa ajili ya mazishi,” amesema Simon Mwakifamba

Kwa upande mtoto wa Mzee Majuto, Ashrafu amesema,ratiba kamili ya mwili wa Mzee Majuto ni kwamba asubuhi  mwili utaandaliwa katika Hospitali ya  Muhimbili na shughuli zote ndogo ndogo zitafanyika hapo, baada ya hapo mwili utapelekwa Karimjee kwa ajili ya kuagwa saa nane mchana," anasema.

Akielezea saa za mwisho za Mzee Majuto Ashrafu anasema: “Hali yake ilibadilika majira ya saa 9.00 alasiri jana hivyo kuhamishwa kutoka jengo la Sewahaji kwenda ICU. Ilipofika saa 1.30 jioni hii hali yake ilibadilika zaidi na madaktari walijitahidi kuokoa maisha yale bila mafanikio. Ilipofika saa 2 usiku alifariki,''

Amri Athuman’ King Majuto’ alizaliwa 1948 jijini Tanga na kusoma shule Msambweni, Tanga, alianza kuigiza 1958 akiwa na umri wa miaka tisa akiigiza katika majukwaa.

Mzee Majuto ambaye alikuwa mtunzi, muigizaji, mwandishi wa mswada na pia ndiye muigizaji wa kwanza kuandaa kazi zake katika mikanda na kuuza akiwa na Tanzania Film Company (TFC).

Soma Zaidi: