Nape, Makamba, Bashe watoa ya moyoni kujiuzulu kwa Kinana

Muktasari:

Kikao cha NEC kiliridhia Kinana kujiuzulu mrithi wake atatajwa leo.


Dar es Salaam. Ni Kinana kila kona.

Jana, Mei 28, Ikulu ilitoa taarifa ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli kuridhia kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana huku akimpongeza kwa uchapakazi wake.

Mara baada ya taarifa hiyo, mitandao ya kijamii ilifunikwa na habari za kung’atuka kwa Kinana kwa kila mmoja kutoa maoni yake kumhusu kiongozi huyo.

Wanasiasa ambao wengi wanatumia mtandao wa twitter, wameonyesha hisia zao mara baada ya taarifa hizo kuwekwa bayana.

Mitandao ya kijamii ilivyofunikwa na habari za kung’atuka kwa Kinana

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameandika katika ukurasa wake wa twitter akisema:

“Pumzika rafiki wa kweli, pumzika mlezi na mzazi usiye mfano, pumzika kiongozi, pumzika komredi. Mwalimu uliyebadili mtazamo wetu juu ya siasa na utumishi kwa umma! tutakuenzi daima! Komredi. Kinana! Umepanda mbegu na itaota.''

Ujumbe huo wa twitter, uliambatana na picha ya Kinana, akiwa pamoja na Nape na Januari Makamba (Waziri anayehusika na Mazingira na Muungano).

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe ameandika: ''Wanakuita Abdul, maana yake mtumishi, wanakuita Abdul Rahmaan, maana yake mtumishi wa Mwenye rehema, Najua umestaafu ukatibu mkuu na si  uana- CCM. Huu ndio uimara wa chama chetu kila kiongozi huondoka na kuacha alama yake. Ila mwalimu hastaafu ualimu wake.”

Kwa upande wake, Makamba, ameandika: ''Hajastaafu bali analitumikia taifa tena bila bughudha za nafasi ya kisasa. Asante kwa elimu kubwa.''