BARAZA LA SALIM: BoT ifanye tathmini utambuzi wa noti bandia

Si mara moja au mbili kuhoji mwenendo wa utendaji kazi, hasa wa kutoa elimu, wa baadhi ya idara na taasisi za serikali.

Mambo yanayofanyika huniacha kwenye kiza na kujiuliza: Hivyo hawa wanaopanga au kufanya mambo hayo wanaielewa jamii yetu na njia nzuri za kuleta

tija kwa elimu wanayotoa?

Kwa mfano, hivi karibuni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilikuwa na mpango mzuri wa kuelimisha jamii njia za kubaini tafauti za noti halisi na bandia.

Hii ni hatua nzuri hasa ukitilia maanani kujitokeza kwa wajanja katika siku za karibuni kutengeneza noti bandia na kuziingiza sokoni, hali iliyopelekea watu wengi kupata hasara.

Lakini sidhani kama waliopewa elimu hiyo ndiyo hasa wale waliostahiki na iwapo hatua hiyo itakuwa na tija

inayotarajiwa.

Nasema hivi kwa sababu hivi karibuni maofisa wa BoT walitoa mafunzo maalumu Zanzibar ya kuelewa ipi noti halisi na ipi ya bandia kwa masheha (wawakilishi wa serikali katika mitaa na vijiji.

Si vibaya hawa masheha kupatiwa elimu hii, lakini nadhani lipo kundi kubwa liliostahili kufikiriwa kwanza kuelimishwa kwa vile ndio hasa wanaotumiwa kuzipenyeza hizi noti bandia.

Kila nikijaribu kuitafuta mantiki ya masheha kupewa umuhimu wa kupata elimu hii siioni hasa kutokana na ninavyoelewa kuwa ni masheha wachache wana uhusiano wa mawasiliano ya karibu na watu wa maeneo wanayoyasimamia.

Wengi wa hawa huwepo majumbani kungojea watu wanaotaka barua za kupata vitambulisho, hati za usafiri, leseni ya biashara au kusaidia kutatua matatizo ya kijamii kama ya majirani waliogombana au ndoa zenye matatizo.

Wachache ndio huwa na mikutano ya mara kwa mara na watu wa maeneo yao na kutokana na mivutano ya kisiasa iliyopo Zanzibar hata wakiitisha mikutano ni watu wachache wanaofika kuwasikiliza.

Kundi linalostahiki kupewa kipa umbele kupata elimu hii ni la wafanya biashara wakubwa na wafanyakazi wa maeneo yanayopokea fedha nyingi baada ya kila dakika chache.

Miongoni mwao ni wafanyakazi wa vituo vya mafuta, washika fedha wanaopokea malipo ya ada kama za kulipia umeme na maji au kukata tiketi za usafiri na wanaoendesha mnada kama ya mifugo au samaki na wanaouza vinywaji katika mabaa au wenye hudumas za kifedha mtandaoni.

Nadhani kundi kubwa la watu hawa niliowataja badala ya masheha ndiyo waliostahiki kwanza kupewa elimu hii ili kuziba mwanya unaotumiwa kirahisi na hawa matapeli kuingiza hizi fedha bandia katika mzunguko hasa nyakati za usiku.

Elimu hii ikitolewa kupitia vyombo vya mbalimbali vya habari kila pembe ya nchi itawasaidia sana wananchi wengi kutokuwa rahisi kupokea noti bandia.

Kwa bahati mbaya wengi wa wafanyakazi wanaopekea mamilioni ya shilingi kwa siku hawana mashine zinazoweza kuwasaidia kugundua ipi fedha safi

na ipi ya bandia na hutegemea zaidi macho ambayo hayana utaalamu wa utambuzi.

Nafikiri viongozi wa BoT wangejipanga upya katika mpango wao wa kutoa elimu ya kugundua fedha bandia.

Miongoni mwa watu wanaoweza kusaidia sana kueneza elimu hii kwa jamii ni waandishi wa habari kwa sababu hili ni kundi la watu linalowasiliana kila siku na wananchi wengi kwa njia mbalimbali.

Kwa muda mrefu tumesikia taarifa kutoka sehemu mbalimbali za Jamhuri ya Muungano ya kuwepo mzunguko wa noti bandia.

Wakati umefika kwa wahusika kufanya tathmini sahihi ya suala hili na kutafuta njia muwafaka za kuidhibiti hali hii ambayo si tu inawatia watu hasara bali pia inahujumu uchumi wa nchi.

Ni vizuri pia pakatolewa taarifa za mara kwa mara juu ya kupatikana kwa hizi noti bandia na kuonyesha kwa umakini katika runinga na maelezo yake kwa kina pia yakasambazwa katika mitandao ya kijamii.

Ni matumaini yangu viongozi wa BoT watatathmini na kutafuta njia nzuri za kutoa elimu hii ya kubaini noti bandia.