Breaking News

MAKALA YA MALOTO: Serikali, Bunge walianza vizuri sakata la Lissu...

Wednesday July 10 2019

 

By Luqman Maloto

Spika wa Bunge, Job Ndugai ameshatangaza kumvua ubunge, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu. Na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) aliyoiandikia imeshatangaza uchaguzi katika Jimbo la Singida Mashariki.

Mjadala uliopo sasa ni uhalali wa uamuzi wa Ndugai. Ndugai amesema Lissu amepoteza sifa ya kuendelea kuwa mbunge kwa sababu hajampa taarifa ya maandishi kuhusu mahali alipo na hajajaza taarifa za mali na madeni yake kama inavyoelekeza Sheria namba 13 ya mwaka 1995, ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kwa maelezo ambayo Lissu mwenyewe ameyatoa, ni dhahiri hajajaza taarifa za mali na madeni yake. Vilevile hajamwandikia barua Spika wa Bunge kuhusu mahali alipo. Angalau hili tukubaliane kwamba Ndugai yupo sawa kwa sababu alizotoa.

Kuuweka vizuri uamuzi wa Ndugai kumvua ubunge Lissu na yale ambayo mwanasiasa huyo amekuwa akiyapitia tangu Septemba 7, 2017, lazima tutofautishe maneno mawili; sawa na sahihi.

Historia ya matatizo ya Lissu yanatuweka kwenye nafasi nzuri ya kutambua kuwa Ndugai yupo sawa kwa uamuzi alioufanya, lakini hayupo sahihi.

Yupo sawa kwa sababu hoja alizotoa kumfuta ubunge Lissu ni za kweli, ila hayupo sahihi kwa sababu kimazingira matatizo ya Lissu yanafahamika.

Advertisement

Septemba 7, 2017, Lissu alipigwa risasi nyingi akiwa kwenye gari nyumbani kwake, akiwa anatokea bungeni. Haya Watanzania wanajua na dunia inatambua.

Tukumbuke siku ya tukio, nchi ilikumbwa na baridi kwa sababu shambulio hilo la aina yake. Mara tu taarifa zilipotoka kuhusu Lissu kushambuliwa, Rais John Magufuli aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter kulaani na kuagiza vyombo vya usalama kuhakikisha wanawatia nguvuni wahusika.

Ndugai alikwenda moja kwa moja Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alipokuwa anahudumiwa Lissu kabla ya kusafirishwa kwenda Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi. Muhimu zaidi ni kwamba alihusika na masuala muhimu ya uamuzi kuhusu matibabu ya mbunge huyo.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu walifika haraka hospitalini Dodoma na kuongeza jitihada za kuokoa maisha ya Lissu.

Aliyekuwa Katibu mkuu Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya ambaye sasa ni balozi, aliingia kazini kutumia utaalamu wake na kushirikiana na madaktari wengine bingwa kuokoa maisha ya Lissu.

Kwa hiyo kulikuwa na ushirikiano mkubwa wakati wa kuokoa maisha ya Lissu.

Mbunge wa Mpendae (CCM), Salim Hassan Turky, alisaidia kupatikana ndege ya dharura, iliyomsafirisha Lissu kwenda Nairobi.

Septemba 8, 2017, wabunge wote walijitolea posho zao za siku na jumla ya Sh40 milioni zilipatikana na kutumwa kwa ajili ya matibabu.

Watanzania wanajua na dunia inajua kuwa baada ya kutibiwa kwa miezi minne Nairobi baadaye kwenda Ubelgiji.

Ukifuatilia mapito hayo na mazingira yake, utaona si kwamba Ndugai hajui alipo. Hata Desemba 2017, alitoa taarifa kwamba angemtembelea hospitali Nairobi baada ya sikukuu za Krismasi mwaka 2017.

Ndugai ndiye aliongoza michango ya wabunge kwa ajili ya Lissu. Wakati anasimamia michango hiyo, tayari mbunge huyo hakuwapo nchini. Na alikuwa na hali mbaya kipindi anasafirishwa, hivyo, asingeweza kuandika barua kuomba ruhusa ya kusafirishwa nje.

Je, ni kweli Ndugai alipanga kwenda Nairobi kumwona Lissu ambaye hakuwa na taarifa zake za maandishi? Pia alikusanya michango ya wabunge kwa ajili ya Lissu ambaye hakutoa taarifa ya maandishi kuhusu mahali alipo? Je, Makamu wa Rais, rais mstaafu, jaji mkuu mstaafu walimtembelea mtu asiyejulikana alipo?

Tangu mvutano wa gharama za matibabu ulipoanza, ilikuwa dhahiri kwamba sakata la Lissu linakwenda kumalizwa vibaya tofauti na lilivyoanza.

Advertisement