Tunaweza kukopa ila tusiuze nchi yetu

Kwa wasomaji wa vitabu na makala mbalimbali za ujenzi wa ufahamu wanatambua namna wataalamu tofauti wa masuala ya ukuaji wa uchumi wanavyozungumzia masuala yanayohusiana na ukopaji.

Baadhi ya wataalamu hawa, hasa wale ambao huishi na mitizamo ya kujitegemea kwa Afrika, huamini kuwa Afrika inapaswa ijitegemee kiuchumi ili isiwe ombaomba au wakala wa mataifa tajiri, hupenda sana kuzungumzia namna ya kukopa, madeni mazuri na mabaya na ukomo wa kukopa.

Katika maisha ya kawaida ya mwanadamu kila mmoja wetu hukopa kulingana na uwezo alionao au hukopa ili kutenda kitu ambacho mwisho wa siku kitamfanya alipe mkopo wake kwa wakati na kwa utaratibu usio na madhara kwake.

Msingi wa Mjadala

Mjadala unaoendelea kwenye taifa letu kuhusu ujenzi wa bandari ya kisasa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani unaweza kuwa sababu ya makala hii. Katika siku za karibuni mradi huu umeibuliwa bungeni Dodoma, ambapo Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameieleza Serikali umuhimu wa mradi huo na kuisisitiza ilete maelezo ya kina ya kwa nini mradi huo hauongezewi nguvu inayostahili.

Lazima pia tuendelee kukubaliana kuwa Ndugai naye ana lengo na nia nzuri, anashangaa ni kwa nini mradi mkubwa kabisa wa kiuchumi unaachwa kando au haupelekwi kwa nguvu wakati jambo hilo lingeweza kufanyika kwa wakati kwa masilahi ya Taifa.

Kwa mtu ambaye si Serikali na siyo Spika Job Ndugai kama mimi, masilahi ya Taifa kwenye eneo la bandari yamo kwenye maeneo matatu, eneo la kwanza ni tija ya ujenzi wa bandari hiyo, eneo la pili ni mkataba wa ujenzi wake na eneo la tatu ni gharama za ujenzi na namna zitakavyolipwa.

Katika eneo la kwanza, nadhani wote watatu, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Rais John Magufuli na Spika Ndugai wanakubaliana kwamba ni jambo la muhimu kwa Tanzania kuwa na bandari ya kipekee – umuhimu huu unaweza kuendelezwa kwa kujenga bandari mpya kubwa kama hii inayopigiwa chapuo Bagamoyo ama kuhuisha bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na kuzifanya kuwa bandari kubwa za kimataifa.

Hatua zote mbili ni sahihi sana, kinachotafutwa na wadau wa maendeleo ni kuona Tanzania inakuwa kinara wa masuala ya bandari katika ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara, jambo ambalo linawezekana – mjadala unaweza kuendelezwa, lakini hauna budi kujikita kwenye suala la msingi la umuhimu wa kuwa na bandari.

Mkataba wa ujenzi wa bandari

Taifa letu limekuwa likiumizwa na mikataba isiyo na masilahi ya Taifa kila mara, ikiwa tunaamua kujenga bandari mpya Bagamoyo kwa kutumia fedha za marafiki zetu wa China na au ikiwa wao watajenga kwa fedha zao na bila kutuomba senti tano, je, wakimaliza ujenzi watatukabidhi bandari yetu na kurudi zao China.

Ukweli ni hapana, ni lazima jambo hili linafanywa kimkataba na katika mkataba viko vipengele ambavyo vinawalinda hawa watakaowekeza matrilioni ya fedha ili Taifa letu lipate bandari. Wachina ni marafiki zetu wazuri lakini mikataba yote ambayo wameingia na mataifa yote duniani katika miradi ya pamoja, ya ufadhili wao na ile ambayo wanajenga ili waiendeshe wao lazima kunakuwa na kipengele kinacholinda masilahi yao, moja ya vipengele vya namna hiyo vimewahi kuzidhuru nchi nyingi za Afrika zikiwemo Zambia na Malawi.

Kama Serikali ingeliweka hadharani vipengele muhimu vya mkataba unaoweza kupelekea kukawa na ujenzi wa bandari hiyo (andiko la awali la mkataba) tunaweza kushangaa kuwa huenda yaleyale ya Zambia na Malawi yanaweza kuhamia Tanzania. Na kwa sababu nchi yetu ina historia ya kuingia mikataba mingi mibovu ni muhimu sana huu wa ujenzi wa bandari ukakaguliwa na tukajiridhisha sana kwamba utakuwa mradi wenye tija ndani ya muda mfupi na muda mrefu.

Mkopo au hisani?

Bandari hii itajengwa kwa fedha za mkopo, yaani Wachina watatupatia fedha za mkopo ili tujenge sisi wenyewe au labda kukiwa na sharti la kutumia kampuni za nchini kwao? Mkopo huo ni nafuu au ghali?

Au je, Wachina wanataka kujenga bandari na kukamilisha mradi huo wao wenyewe kwa fedha zao kisha watukabidhi sisi tuuendeshe na wao wakiwa wabia wa uendeshaji na kisha kila mara tugawane faida na wao wakitumia faida ya mwanzo kama malipo ya deni lao?

Na je, kama Wachina watatujengea kwa gharama zao na kisha tukaanza kuiendesha bandari kiubia, ubia huo utakuwa wa muda gani? Miaka 10? 30? 50? 100? Ubia huo utakuwa na madhara gani kwa nchi?

Vipi kuhusu uwiano wa gharama za mradi husika dhidi ya uwezo wa nchi kibajeti na kiukopaji? Kwa mfano, Taifa lako linajiendesha kwa bajeti ya Sh30 trilioni kwa mwaka, unaweza kukopa au kusaidiwa kujenga mradi mmoja wa Sh20 trilioni?

Yaani theluthi mbili ya bajeti yako ya mwaka mzima? Je, ikitokea mradi wa bandari haulipi (hauleti marejesho yanayotakiwa kwa sababu mbalimbali), matrilioni hayo ya fedha ambazo Wachina watakuwa wametumia kujenga bandari yatalipwaje? Kwa utaratibu gani?

Ni muhimu tukajifunza kukopa lakini siyo kukopesha nchi zetu kwa wageni au mataifa mengine. Tuendelee kukopa lakini tusikope na kuliweka Taifa rehani, rehani mbaya!

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtaalamu Mshauri wa Miradi, Utawala na Sera. Pia Mtatiro ni Mtafiti, Mfasiri na Mwanasheria. Simu; +255787536759 \ Barua Pepe; [email protected])