Tajiri wa mabasi ya Zakaria ahojiwa kwa tuhuma za kuwapiga risasi maofisa usalama

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe

Muktasari:

Ingawa mazingira ya tukio hilo na nini maofisa hao walifuata kwenye kituo cha mafuta kinachomilikiwa na mfanyabiashara huyo hayajajulikana, mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema jana mjini Musoma kuwa, tukio hilo lilitokea saa mbili usiku wa Juni 29.

Musoma/Tarime. Mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Zakaria, Peter Zakaria anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kwa tuhuma za kuwajeruhi kwa risasi watu wawili wanaodaiwa kuwa ni maofisa usalama wa Taifa.

Ingawa mazingira ya tukio hilo na nini maofisa hao walifuata kwenye kituo cha mafuta kinachomilikiwa na mfanyabiashara huyo hayajajulikana, mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema jana mjini Musoma kuwa, tukio hilo lilitokea saa mbili usiku wa Juni 29.

Malima alisema baada ya kuwajeruhi kwa risasi maofisa hao, Zakaria alidhibitiwa na maofisa wengine ambao walimfikisha Kituo cha Polisi mjini Tarime.

Akifafanua, mkuu huyo wa mkoa alisema kabla ya tukio hilo, maofisa usalama watano walifika katika kituo hicho cha mafuta kwa nia kujaza mafuta gari lao, ndipo wenzao wawili walishuka na ghafla kushambuliwa kwa risasi.

“Baada ya wenzao kujeruhiwa kwa risasi, maofisa wengine walifanikiwa kumdhibiti Zakaria na kumtia mbaroni na kumkabidhi kwa polisi wanaoendelea kumhoji,” alisema.

Kwa mujibu wa Malima, maofisa waliojeruhiwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwa matibabu huku mmoja akidaiwa kuwa katika hali mbaya.

Kuhusu tukio la polisi kutumia mabomu ya machozi kuutawaanya umati wa wananchi waliokusanyika eneo la hospitali hiyo, kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema lililenga kurejesha utulivu baada ya wananchi kuhamaki wakitaka kuingia kumuona Zakaria kutokana na kuzagaa taarifa kuwa amejeruhiwa na kulazwa.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wafanyakazi wa kituo cha mafuta, alidai Zakaria alifyatua risasi ili kujihami baada ya kuhisi kuwa watu walioshuka kwenye gari wakielekea ofisini kwake walikuwa majambazi.

“Kwa kawaida muda ule bosi huwa anapokea fedha za mauzo kutoka sehemu mbalimbali za biashara zake ikiwamo mabasi na vituo vya mafuta. Kitendo cha watu watano kufika na wawili kushuka kuelekea ofisini kwake kiliibua hofu ya usalama kutokana na matukio ya ujambazi, ndipo akaamua kujihami,” alisema mfanyakazi huyo.

Alisema baada ya wenzao kujeruhiwa, watu watatu waliobaki kwenye gari waliteremka na kumkamata Zakaria huku wakijitambulisha kuwa maofisa usalama, hali iliyozua mvutano walipotaka kuondoka naye kwa sababu wafanyakazi hawakuwa na uhakika iwapo walikuwa wema au wahalifu.

Mvutano huo ulisababisha milio ya risasi na watu hao kuondoka na Zakaria kwa nguvu huku wakisababisha hofu kuwa huenda mfanyabiashara huyo ametekwa, jambo lililoibua taharuki mjini Tarime.