Tido: Tuhuma hizi zimeniumiza sana

Muktasari:

  • Tido anayekabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati akiongozwa na wakili Martine Matunda na Ramadhani Maleta kutoa ushahidi wake wa utetezi katika kesi inayomkabili.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando amesema Serikali imelipa Sh887.1 milioni kwa watu wasiojulikana tofauti na inavyodaiwa na upande wa mashtaka akisema tuhuma hizo zimemuumiza sana.

Tido anayekabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati akiongozwa na wakili Martine Matunda na Ramadhani Maleta kutoa ushahidi wake wa utetezi katika kesi inayomkabili.

Katika utetezi wake, Tido aliyetumia saa tatu kujitetea alidai kuwa alikwenda kufanya kazi TBC baada ya kuitwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na majukumu yake yalikuwa ni kulibadilisha shirika hilo liwe lenye uwezo na kuheshimika duniani.

Alidai kuwa tuhuma zinazomkabili zimemuumiza sana kwa sababu alikuwa na ndoto ya kuifikisha TBC mbali ili iweze kutoa gawio kwa Serikali na si Serikali kutoa fedha kwa TBC.

Kuhusu kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni, Tido alidai hakushirikishwa kwa namna yoyote katika malipo hayo na angeshirikishwa angeweza kunusuru fedha hizo zisilipwe.

Alidai kuwa mwaka 2012, aliitwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoa maelezo na malipo yanaonyesha kufanyika mwaka 2015 yeye akiwa tayari ni mtuhumiwa na hakuwahi kuitwa popote kuulizwa kuhusu mchakato mzima wa mradi kabla malipo hayo hayajafanyika kwani angeweza kushauri.

Tido aliyeanza kujitetea saa tatu asubuhi hadi saa sita mchana, aliieleza Mahakama kwamba yeye kitaaluma ni mwandishi wa habari, kazi aliyoifanya kwa miaka 50.

Alidai akiwa mkurugenzi mkuu wa TBC alikuwa akiripoti kwa bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo na anaufahamu mradi wa mabadiliko ya teknolojia ya utangazaji kutoka mfumo wa analojia kwenda digitali.

Tido alidai kuwa walifahamu muda mrefu na kwamba wahusika wakubwa walikuwa ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na TBC kama shirika la umma walikuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wake.

Alieleza mahakamani hapo kuwa walishirikishwa katika vikao mbalimbali vya awali na wakati huo walipewa ishara ya maandalizi ya kuhakikisha wakati ukifika utekelezaji unaanza ipasavyo.

Akiendelea kujitetea, Tido alidai kuwa kwa kuangalia maeneo mengine, shida kubwa za nchi za Afrika zilikuwa ni kuwapata watu kwenye uwezo wa kutekeleza mradi huo.

Alisema Tanzania kupitia TBC kulikuwapo na mazungumzo kwa kipindi kirefu kwa sababu TCRA walikuwa wanataka kuiachia jukumu TBC.

“Hivyo ikaamuliwa kuwa na aina tatu za wale wanaosimamia urushaji wa matangazo hayo ya digitali,” alisema

Alisema kutokana na ukubwa wa mradi huo, TBC ndiyo ilitegemewa kuwa inauongoza hivyo iliruhusiwa kutafuta mbia mwenye uwezo wa kifedha wa kuendesha.

Tido alisema mahakamani hapo kuwa akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC ili kufanikisha mchakato huo wa kuhamia digitali walianza kuzungumza na watu hata kwenye mikutano kila walipopata nafasi.

Alibainisha kampuni za kimataifa zilizokuwa na hadhi ambayo ilikuwa inatakiwa zilikuwa chache na zilikuwa na malengo ya kupata faida na kwamba hiyo ilikuwa ni changamoto.

“Tulifanikiwa kupata kampuni tatu, kampuni ya Uswiss, kampuni ya Channel 2 Group ya Dubai na kampuni ya Startimes nao walikuwa na matakwa yao mbalimbali,” alisema.

Alidai kuwa kampuni ya Uswiss ilionyesha mapema kuwa tayari imepata nafasi nzuri Afrika Magharibi katika nchi za Nigeria na Ghana hivyo ikajiondoa na hata walipopelekewa mwaliko hawakujibu.

“Kampuni ya Channel 2 Group wao walitaka kuhakikishiwa kama watashirikishwa katika mchakato na kwamba wafanye makubaliano ya awali hivyo waliandikishana na kuwaambia utakapofika wakati wa mchakato wasiwe na wasiwasi,” alisema.

Tido alidai kuwa katika maandishi hayo yeye alisaini na kwa upande wa Channel 2 Group alisaini mmiliki wake Sethi Dubai na kwamba alifanya hivyo kwa kuzingatia kuwa hayo yalikuwa makubaliano ya mwanzo.

“Tangu nimekaa TBC sijawahi kupokea malalamiko yoyote kutoka kwa mmiliki wa Channel 2 Group Sethi,” alisema Tido.

Tido alidai kuwa fedha hizo zinazodaiwa kulipwa kwa mawakili wa Uingereza katika kesi iliyofunguliwa huko zililipwa kusiko julikana.

Tido alidai mahakamani hapo kuwa aliifanya kazi kwa utulivu ufanisi na weledi katika utekelezaji wa mradi huo na kuliletea taifa sifa.

Tido alieleza kuwa iwapo angeshirikishwa kuhusu kesi hiyo iliyofunguliwa Uingereza ambayo aliisikia katika ushahidi wa upande wa mashtaka, angeweza kutoa ushauri na hata hayo matumizi ama yasingekuwapo au yasingefanyika bila mpangilio.

Wakili wa Takukuru Swai aliiomba mahakama impe nafasi ili aweze kujiandaa kumhoji Tido dhidi ya ushahidi alioutoa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 9.