Upande wa mashtaka kumhoji Tido Oktoba 16

Muktasari:

Ni katika kesi anayotuhumiwa kutumia vibaya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.

Dar es Salaam. Oktoba 16, 2018 aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando ataanza kuulizwa maswali na upande wa mashtaka dhidi ya utetezi alioutoa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Tido anatuhumiwa kwa kutumia madaraka vibaya na kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.

Alitoa utetezi wake dhidi ya mashtaka hayo Septemba 20, 2018 akiongozwa na mawakili wake, Dk Ramadhani Maleta na Martin Matunda.

Hatua hiyo ilipaswa kufanyika leo Jumanne Oktoba 9, 2018 lakini ilishindikana baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kuwa na udhuru.

Kufuatia udhuru hiyo, wakili Emmanuel Mtumbe aliyemwakilisha  Swai mahakamani hapo aliiomba kuahirishwa kwa shauri hilo -  ombi ambalo liliridhiwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 16 ambapo Tido ataanza kuulizwa maswali na upande wa mashtaka dhidi ya utetezi wake alioutoa.

Tido alianza kujitetea baada ya upande wa mashtaka kuwaita mashahidi wao kutoa ushahidi na kuufunga.

Miongoni mwa  mashahidi  hao ni ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya;  mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa;  Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana na  Dominic Maundi. 

Katika kesi hiyo inadaiwa Juni 16, 2008,   akiwa  Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na sheria ya manunuzi ya umma na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa dijitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa  Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho  anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh887,122,219.19. Tido yupo nje kwa dhamana.