Upelelezi kesi ya mke wa Bilionea Msuya haujakamilika

Muktasari:

Kesi hiyo inamkabili mke wa Bilionea Msuya, Miriam Mrita akidaiwa kuhusika na mauaji ya dada wa Bilionea Msuya, Aneth Msuya.


Dar es Salaam. Upande wa Mashtaka katika kesi ya mauaji inayomkabili mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita (41), umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Frola Masawe amedai leo, Septemba 6, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Mbali na Mrita, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ya mauaji namba 5 ya mwaka 2017 ni mfanyabiashara Revocatus Muyela (40) na wote wanakabiliwa na shtaka mmoja la mauaji ya dada yake Erasto Msuya, Aneth Msuya.

"Shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika, hivyo tu naomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" amedai Frola.

Baada ya Frola kueleza hayo, Wakili wa utetezi Omari Msemo kwa niaba ya Peter Kibatala aliomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wao kwa wakati.

Kutokana na maelezo ya pande zote, Hakimu Simba, aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa wanakamilisha haraka upelelezi katika shauri hilo kwani Kesi hiyo ni ya muda mrefu.

"Ni Kesi ya muda mrefu, washtakiwa wamefikishwa mahakamani hapa kwa mara  ya kwanza, Februari 24, 2017 na mpaka leo, upelelezi bado, nataka upande wa mashtaka mhakikishe mnakamilisha upelelezi haraka ili kesi  iweze kuendelea kwa hatua nyingine" amesema Hakimu Simba.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi, Septemba 12, mwaka huu, itakapotajwa.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji, ambapo wanadaiwa kumuua dada wa Bilionea Msuya, Aneth Msuya.

Februari 23, 2017  washtakiwa hao waliachiwa huru na mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa na kisha wakakamatwa tena na baadaye kusomewa shtaka moja la mauaji upya.

Washtakiwa wanadaiwa kumuua kwa makusudi dada wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Aneth Msuya tukio linalodaiwa kutokea Mei 25, 2016, maeneo ya Kibada Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

Soma Zaidi: