Upimaji samaki mgahawa wa Bunge wazua mazito

Muktasari:

Dk Tulia alitoa agizo hilo jana akihitimisha hoja iliyotolewa na mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba iliyojadiliwa na wabunge.

Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameitaka Serikali kuwasilisha taarifa bungeni leo kuhusu maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuingia katika mgahawa wa Bunge kupima samaki wanaodaiwa kuvuliwa haramu.

Dk Tulia alitoa agizo hilo jana akihitimisha hoja iliyotolewa na mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba iliyojadiliwa na wabunge.

Awali, asubuhi maofisa wa wizara hiyo walikamata samaki kilo mbili waliokuwa wakiuzwa kinyume cha sheria katika mgahawa huo.

Samaki hao wenye urefu chini ya sentimita 25 kutoka Ziwa Victoria walikamatwa katika mgahawa wa Lamba Catering Service. Ni kati ya kilo 100 za samaki waliokuwapo mgahawani hapo.

Kaimu meneja Uhifadhi wa Bahari na Maeneo Tengefu wa wizara hiyo, John Komakoma alisema samaki hao kisheria hawapaswi kuvuliwa.

“Mmiliki wa mgahawa amekiri kosa na kisheria tumemtoza Sh300,000 atakazokwenda kulipia benki,” alisema Komakoma.

Msemaji wa wizara hiyo, John Mpepele alisema aliyewapa taarifa za kuwapo samaki hao ni waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliyekwenda mgahawani jana asubuhi. “Alipowaona samaki hawa alitia shaka akatuagiza kuja kufuatilia,” alisema.

Mmiliki wa mgahawa huo, Daniel Labiaramba alisema anakiri kosa lakini ni vigumu kwake kujua kama kulikuwa na samaki hao kati ya kilo 100 alizonunua. “Sikufanya hivi makusudi, kwani sikujua,” alisema.

Katika mjadala bungeni, wabunge walimtaka Mpina na naibu wake, Abdallah Ulega kuwaomba radhi wabunge ikiwamo kuchukuliwa hatua kali wakisema wamelifedhehesha Bunge.

Serukamba akitumia kanuni ya 47 kutoa hoja alisema, “Leo wamekuja maofisa, wakaenda canteen (mgahawani), wakaenda jikoni wakapima samaki walioandaliwa. Maofisa wamekuja bungeni hawakumwambia spika, hawakumwambia katibu wa Bunge wala wewe naibu spika.”

“Bunge hili haliko salama, canteen ile wanakula wabunge, wale waliokuja wamekuja kwa nia gani, wanaokuja si wanakuja wanapiga hodi, naomba tulijadili hili hao maofisa tujue wamepata wapi hayo madaraka, wanalishusha hadhi Bunge lako tukufu.”

Dk Tulia aliiruhusu hoja hiyo iliyochangiwa na wabunge wa kwanza akiwa wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea aliyesema mara kadhaa imeshuhudiwa unyanyasaji wa maofisa wa Serikali dhidi ya wananchi.

“Leo wabunge tunakula chakula, usalama wetu uko wapi, jambo hili halikubaliki na lazima washughulikiwe hawa watu,” alisema.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Cecilia Paresso alisema Bunge ni lazima liangalie usalama wa wabunge akishauri watumishi waliofanya kitendo hicho lazima wachukuliwe hatua.

Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema wameacha wenyewe heshima ya mhimili huo imomonyoke kwa wabunge kukamatwa na polisi bila taarifa kwa Bunge au spika.

“Taasisi zingine wameachwa wanafanya wanavyotaka, leo wanashika katika mazingira gani? Hapa tulipofikia mlaji wa mwisho samaki amepikwa yuko jikoni, naungana na Serukamba watu hawa waitwe kamati ya nidhamu wahojiwe na walikujaje humu na kufanya nini, mwenyeji wao ni nani na kujua huo mlolongo wote,”alisema

Mbunge wa Mkinga (CCM), Dunstan Kitandula alisema iwapo waliingia bila kupata ruhusa Bunge lichukue hatua haraka, huku mbunge wa Kilolo (CCM), Venance Mwamoto akisema utaratibu wa wageni kuingia ndani ya Bunge unafahamika.

Wabunge wengine waliochangia hoja hiyo ni wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi; wa Serengeti (Chadema), Ryoba Chacha na wa Liwale (CUF), Zuberi Kuchauka.

Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almasi Maige alisema, “Haiwezekani Serikali kuja kupima samaki bungeni hii ni kuvuana nguo, leo usalama wetu umeguswa na haujawahi kuguswa na kama wametumwa na waziri, basi waziri huyu ana bidii na hana busara na waziri huyu hayuko na Rais.”

Pia, hoja hiyo ilichangiwa na mbunge wa viti maalumu (Chadema), Dk Immaculate Sware na wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu.

Akihitimisha hoja yake, Serukamba alisema, “Nashukuru Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) upo, tunakuomba ufanye uamuzi kwa kiongozi huyu wa wizara hii, waziri huyu aende katika kamati ya maadili na maofisa wake na Bunge hili lifanye uamuzi na tusipofanya uamuzi, hatutaheshimiwa tena na Serikali.”

Naibu spika akihitimisha hoja hiyo, alisema kwa kuwa Waziri Mkuu, Majaliwa alikuwapo, leo Serikali iwasilishe taarifa ya jambo hilo bungeni.

“Baada ya kuleta taarifa hiyo, tupate muda wa kuchambua suala hilo. Namna lilivyotokea ili Bunge liweze kufanya uamuzi,” alisema.