Utata wa kisheria wamzuia Bulaya kutoa ushahidi

Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.

Muktasari:

Hatua hiyo ilitokana na malumbano ya kisheria kati ya mawakili wa upande wa waleta maombi na wa utetezi hali iliyosababisha Jaji Noel Chocha anayesikiliza kesi hiyo kuiahirisha hadi leo mchana.

Musoma. Utata wa kisheria umemkwamisha Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya kutoa ushahidi katika kesi ya kutetea ubunge wake inayoendelea mjini Musoma.

Hatua hiyo ilitokana na malumbano ya kisheria kati ya mawakili wa upande wa waleta maombi na wa utetezi hali iliyosababisha Jaji Noel Chocha anayesikiliza kesi hiyo kuiahirisha hadi leo mchana.

Utata huo uliibuka baada ya wakili Constantine Mutalemwa wa upande wa waleta maombi kuweka pingamizi katika baadhi ya aya kwenye hati ya kiapo cha shahidi huyo hatua iliyozua mjadala mkubwa kati yake na wakili wa upande wa utetezi Tundu Lissu.

Katika mjadala huo mahakani jana, kila wakili alijaribu kutetea hoja yake na kutoa vifungu vya sheria ambavyo vinaonyesha msingi wa hoja walizokuwa wakitoa.

Wakili Mutalemwa alisema aya hizo ambazo aliiomba mahakama ziondolewe zilikuwa zinapingana na matakwa ya kanuni na sheria za kuongoza mashauri ya kesi za madai ya uchaguzi.

Mutalemwa alisema kati ya aya 11 zilizosomwa na mjibu maombi wa kwanza katika kiapo chake zinazotakiwa kubaki katika kiapo hicho ni aya nne ambazo alisema hazina utata wowote.

Alizitaja aya ambazo zilitakiwa kuondolewa kwenye kiapo hicho cha shahidi wa kwanza kuwa ni pamoja na aya ya 2,3,4,5,6,7,8 ambazo zilikuwa zinaibua hoja mpya ambazo hazikutajwa kwenye majibu yao wakati wakijibu maombi katika hatua za awali. Hata hivyo, hakufafanua kilichomo kwenye aya hizo.

Kutokana na mjadala huo wa kisheria, Jaji Chocha aliamua kuahirisha kesi hiyo ili kwenda kupitia hoja hizo kabla ya kufanya uamuzi utakaotolewa leo.