VIDEO-Nyalandu alivyoeleza kwa nini ameachia ngazi

Muktasari:

Nyalandu ameeleza hayo leo Jumatatu kuwa ameamua  kujiuzulu nafasi yake ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za uongozi ndani ya chama hicho kuanzia leo Jumatatu, Oktoba 30.

 Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu amefunguka mwanzo mwisho kwa nini ameamua kujiuzulu ubunge wake na kuihama CCM.

Nyalandu ameeleza hayo leo Jumatatu kuwa ameamua  kujiuzulu nafasi yake ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za uongozi ndani ya chama hicho kuanzia leo Jumatatu, Oktoba 30.

Amesema mbali na hilo asubuhi ya leo Jumatatu amemwandikia Spika wa Bunge,Job Ndugai barua ya kujiuzulu nafasi yake ya ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo ameitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2000 hadi sasa.

“Nimechukua uamuzi huo kutokana na kutorishwa kwangu na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya Watanzania wenzetu na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya mihimili ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa kibunge wa kutunga sheria na wa kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana kikatiba,”

“Vilevile, naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya sasa, hakuna namna yoyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na Mahakama ambayo ndio chimbuko la uongozi bora wa nchi na kuonyesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe na kwamba Serikali ni ya watu kwa ajili ya watu.”

Amesema yeye anaondoka anaondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa amekitumikia kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, ujumbe wa kamati ya wabunge wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kwani amejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali.

“Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna moja au nyigine, CCM nayo imekuwa chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,”

“Hivyo basi kwa dhamira yangu na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na haki ya kikatiba natangaza kukihama Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii na nitaomba ikiwapendeza wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) basi waniruhusu kuingia malangoni mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na Chadema na Watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa kidemokrasia na uhuru wa mawazo.”

Amesema ameamua kujiuzulu kiti cha ubunge, jimbo la Singida Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua itikadi wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki nchini Tanzania.

“Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba, sote kama Taifa tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu. Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa haki itamalaki Tanzania. Upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za kisiasa na makabila yote nchini uimarike. Tushindane kisera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu na Taifa lililo imara na nchi yenye adili.”