VIDEO-Naibu waziri wa zamani apoteza ndugu 13 ajalini

Muktasari:

  • Rais John Magufuli ametuma rambirambi kutokana na vifo hivyo.

Watu 13 waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea nchini Uganda imefahamika kuwa wana uhusiano na naibu waziri na mbunge wa zamani wa Mpwapwa mkoani Dodoma, Gregory Teu.

Tayari Rais John Magufuli amemtumia rambirambi Teu aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Nne kutokana na vifo hivyo akisema ni ndugu wa familia yake.

Vifo vyao vimetokana na basi walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye sherehe ya harusi kugongana na lori jana Jumapili saa nne usiku katika Barabara ya Masaka nchini Uganda wakiwa njiani kurejea nchini.

 “Nimepokea taarifa ya vifo hivi kwa mshtuko mkubwa, nimehuzunishwa na kuondokewa na idadi hii kubwa ya watu. Nampa pole Gregory Teu kwa kufikwa na msiba huu mkubwa, nawapa pole wanafamilia, ndugu na jamaa wote walioguswa na vifo hivi,” amesema Rais Magufuli.

Katika taarifa ya Ikulu amesema, “Nawaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema na pia nawaombea majeruhi wote wanaopata matibabu nchini Uganda wapone haraka na kurejea nyumbani.”

Rais Magufuli amewataka wanafamilia kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea.