Viongozi wa dini waingilia suala la umri wa Rais Uganda

Muktasari:

  • Wataka mjadala muhimu kama huo uamliwe kwa kura ya maoni
  • Wataka vyombo vya usalama viache kunyanyasa wanaopinga hoja
  • Pia wataka Rais Museveni aonyesha ukomavu wa kiutawala

Baraza la Viongozi wa Dini nchini limetoa wito kwa serikali kuruhusu hoja ya ukomo wa umri wa rais iamriwe na wananchi wote kwa kupiga Kura ya Maoni.

Baraza hilo linalojumuisha wakuu saba wa madhehebu makubwa ya dini nchini limesema katika taarifa yao ya pamoja wiki iliyopita kwamba watu waruhusiwe kuamua hatima yao.

Mjadala kuhusu kuondolewa kwa ukomo wa umri wa rais si suala la upande mmoja ambalo linahodhiwa na wanasiasa na au wabunge...wananchi wana maoni tofauti kuhusu sauala hilo, hivyo kuna haja ya kusikiliza kwa utulivu pande zote bila ya kuegemea upande mmoja na kuutisha mwingine.

Walipendekeza Mjadala wa Taifa uandaliwe kuhusu ukomo wa umri wa rais na baadaye ifanyike kura ya maoni.

Walitoa wito kwa vyombo vya usalama “kuacha kuwasumbua watu wa upande mmoja na kupendelea mwingine (yaani upande unaopigania ukomo uondolewe na unaopinga).”

Baraza hilo pia limetoa wito kwa Rais Yoweri Museveni “kuonyesha ukomavu wa kiutawala katika suala hili”.

Hivi karibuni wabunge wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) na wa kujitegemea walipitisha uamuzi wa kuondolewa ukomo wa umri wa miaka 75 uliowekwa katika Katiba.

Ikiwa marekebisho hayo yatapitishwa bungeni, itakuwa na maana kwamba Rais Museveni mwenye umri wa miaka 73 sasa ataweza kugombea uchaguzi ujao mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 77. Mwaka 2005, katiba ilifanyiwa marekebisho ukaondolewa ukomo wa mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.