Wabunge wahoji juu ya orodha ya ‘wauza unga’ ya Kikwete

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe

Muktasari:

Akichangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Ukimwi na ile ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema Rais Kikwete aliwahi kuutangazia umma kuwa anayo orodha ya vigogo wa dawa za kulevya hivyo alitaka wakamatwe ili watumiaji waachiwe.

Dodoma. Sakata la dawa za kulevya jana lilitikisa Bunge mjini hapa baada ya wabunge kutaka orodha ya ‘wauza unga’ ambayo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema anayo ili ifanyiwe kazi na mrithi wake, John Magufuli.

Akichangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Ukimwi na ile ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema Rais Kikwete aliwahi kuutangazia umma kuwa anayo orodha ya vigogo wa dawa za kulevya hivyo alitaka wakamatwe ili watumiaji waachiwe.

“Kikwete alisema anayo orodha ya wauza dawa za kulevya. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Mwigulu Nchemba) amfuate kule Msoga ili ampe hiyo orodha. Naamini watumiaji wataachiwa,” alisema.

“Vita ya dawa za kulevya siyo ya Paul Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam), hii ni vita ya Serikali na naamini itamuunga mkono. Mtu akipimwa akionekana ni mtumiaji atusaidie kumpata muuzaji,” alisema.

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alimtaka Rais Magufuli kuacha kuendesha nchi kwa sanaa na kutafuta habari zake zipewe uzito katika vyombo vya habari, badala ya kushughulika na tatizo.

Mbunge huyo alisema kwa mwaka 2016/2017, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini ambayo ndiyo yenye dhamana ya vita hiyo haikupata fedha za maendeleo. “Leo bajeti ya tume ni sifuri halafu anasimama mkuu wa nchi anasema vita ipiganwe. Tuache kutafuta vichwa vya habari kwenye vyombo habari,” alisema Mdee.

Aliongeza, “Vita hii inahitaji utashi wa kisiasa. Kikwete alisema anawajua wauza unga kwamba ana orodha. Alipoondoka Ikulu si aliacha mafaili? Orodha unayo hapo Ikulu tusicheze na akili za Watanzania,” alisema.