Waliofariki dunia ajali ya MV Nyerere wafikia 94

Muktasari:

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella hadi leo saa 5 asubuhi Septemba 21, 2018 jumla ya maiti 94 zimeopolewa

Dar es Salaam. Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama jana mchana Septemba 19, 2018 imefikia 94 huku uokoaji ukiendelea muda huu.

Akizungumza leo saa 5:30 asubuhi, mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mbozi Katara ametoa taarifa kuhusu zoezi la uokoaji akimnukuu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuwa miili iliyoopolewa imefikia 94.

Leo saa 4 asubuhi Mongella alibainisha kuwa miili 42 imepatikana leo asubuhi, wakati mingine 44 ilipatikana jana.

Kwa kauli hiyo maana yake ni kuwa tangu wakati huo hadi sasa miili minane imeopolewa, kufanya idadi kufikia 94.

Kivuko hicho kilizama katika Ziwa Victoria mita 50 kabla ya kutia nanga kisiwa cha Ukara.

Kilikuwa kikitokea katika Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, kinadaiwa kilikuwa kimepakia zaidi ya abiria 100, wengi wakiwa wanaelekea kwenye gulio.