Wananchi wahoji kusitishwa kwa muda uokoaji ajali ya MV Nyerere

Muktasari:

Kuzama kwa  kivuko cha MV Nyerere imewakumbusha wengi ajali iliyotokea mwaka 1996 ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba  huku watu zaidi ya 800 wakifariki dunia

Dar es Salaam. Kitendo cha kusitishwa uokoaji wa watu waliokuwa katika kivuko cha MV Nyerere kilichozama jana mchana umeibua mjadala mitandaoni, huku wengi wakilaumu uamuzi huo.

Uokoaji huo ulisitishwa jana jioni Alhamisi Septemba 20, 2018 huku miili ya watu 44 ikiwa imepatikana na kuendelea tena leo asubuhi Ijumaa Septemba 21, 2018 ambapo mpaka saa 4 asubuhi miili mingine 42 imeopolewa.

Kivuko hicho kilizama katika Ziwa Victoria mita 50 kabla ya kutia nanga kisiwa cha Ukara.

Kilikuwa kikitokea katika Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, kinadaiwa kilikuwa kimepakia zaidi ya abiria 100, wengi wakiwa wanaelekea kwenye gulio.

Jana Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  John Mongella alisitisha zoezi la uokoaji kutokana na giza sambamba na boti kutokuwa na injini.

Katika mitandao mbalimbali ya kijamii ya kijamii ya Mwananchi, watu waliotoa maoni yao kufuatia ajali hiyo walilaumu uamuzi huo, huku wakihoji kuwa tangu kuzama kwa MV Bukoba mwaka 1996, mamlaka husika hazikuchukua tahadhari.

 

Katika mtandao wa Twitter, Think Different ameandika, “unakosa taa za dharura mkoa mzima? Kamati ya ulinzi wanajadili nini? Haya mambo tuyarudishe kwa majeshi wanasiasa wameshindwa.”

Naye Aydrassally amemuhoji mkuu wa mkoa huo kwa kusema, “Ingekuwa kuna mwanao ungesema zoezi la uokoaji liendelee leo? Hivi mmeingiwa na ushetani gani nyinyi wenzetu,  mbona utu umewatoka kiasi hicho , mlikosa kujiandaa kwa ajili ya usiku huu.”.

Mbaraka Islam amesema “waliositisha shughuli ya uokoaji watakuwa wanasiasa na si wananchi hasa wavuvi ambao hukesha kuvua kwa karabai. Wakati wa ajali ya MV Bukoba mwaka 1996 wavuvi walikesha kuokoa, Mungu tupe subira Watanzania.”

Maria Sarungi amesema, “hata kama ni watu wawili na dimbwi na taa za kuvulia dagaa, lakini Serikali haipaswi kutangaza shughuli ya uokoaji kusitishwa.”

Maria ameshauri uokoaji uendelee usiku na mchana na Serikali iombe msaada kwa watu binafsi na nje ya nchi.

Olemmari amesema, “angalia tunanunua magari ya Polisi na silaha nzitonzito za kulinda watawala, kuliko ambavyo tunanunua vifaa vya kisasa vya kulinda raia na kufanya uokoaji kama hivi.”

Kwa upande wake CWPedro amesema, “hawana la kufanya pale ziwani ni giza kweli kweli. Tangu mwaka 1996 ilipozama  MV Bukoba hakuna tahadhari yoyote tuliyochukua kwa majanga tulidhani ile ndiyo ya mwisho.”

Naye Mangi ameandika, “kauli ya mkuu wa mkoa inakera ...Hivi unawezaje kumwambia mtu ambaye ndugu yake alikuwa kwenye kivuko kuwa umeahirisha zoezi la uokoaji.”

Alphonce Lusako alias Emekha Ikhe: Ameandika “...Nimeshangaa sana Waziri mwenye dhamana mpaka sasa hajatangaza kujiuzulu kwa ajali iliyotabiriwa huko Mwanza, uwajibikaji ziro Tanzania nitashangaa sana kama hatajiuzulu

Ntobi: Ameandika...Nilitegemea kusikia waziri mwenye dhamana anajiuzuru haraka mara baada ya kuenea kwa video ya Mbunge wa Ukerewe Joseph Mkundi ili kuepuka ajali kama hiyo.

Richard Mabala: ameandika...Hivi hakuna mtu anayeweza kwenda kumuamsha mkuu wa mkoa?. Hakuna watu binafsi wa kujitolea kupeleka taa pale lazima zipo jamani watu wapo hatarini kufa.