Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Wanane wafariki, wabunge sita wakinusurika ajalini Moro

WABUNGE SABA WANUSURIKA AJALINI MOROGORO

Muktasari:

Gari la wabunge hao lilipinduka likimkwepa mbwa

Dar/mikoani. Watu wanane wamefariki dunia katika ajali ya basi iliyotokea wilayani Ngara, huku wabunge sita wa CCM na CUF wakinusurika katika ajali iliyotokea eneo la Gwata Maseyu.

Katika ajali ya kwanza iliyotokea juzi, mabasi manane yaliyokuwa yamebeba wakimbizi kutoka kambi ya Nduta, Kibondo, Kigoma yalipinduka na kusababisha vifo hivyo vya watu wanane.

Katika ajali hiyo iliyotokea saa 11 jioni, basi moja kati ya manane yaliyobeba wakimbizi hao lilifeli mfumo wa breki na kuligonga lililokuwa mbele yake na yote kupoteza mwelekeo kisha kupinduka.

Ofisa Mwandamizi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) wilayani Ngara, Irene Babu alisema waliopoteza maisha ni wakimbizi sita na Watanzania wawili.

Kati ya Watanzania hao waliofariki, miongoni mwao ni mwandishi wa habari, Hassan Jureji aliyewahi kufanya kazi katika vituo mbalimbali vya televisheni na redio nchini ikiwamo EATV.

Alisema Mtanzania mwingine ni mfanyakazi wa Shirika la Afya la Kuhudumia wakimbizi (IOM).

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Murugwanza wilayani Ngara, Dk Remmy Andrew alithibitisha kupokewa miili hiyo.

Mganga huyo alisema hospitali hiyo ilipokea majeruhi 65, kati yao, 30 ni wanawake na 35 ni wa kiume. Pia wamo watoto 11 chini ya umri wa miaka mitano.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera, Agustino Olomi alisema waliofariki eneo la tukio ni wanawake watatu na wanaume wawili ambao bado hawajatambulika na idadi kamili ya majeruhi.

Hadi jana, watu wengine watatu walifariki dunia na kufanya idadi ya waliofariki kuwa wanane.

Wabunge sita wanusurika ajali

Wakati masahibu hayo yakitokea Ngara, wabunge sita wa Zanzibar, wamenusurika katika ajali baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka wakati dereva alipokuwa akimkwepa mbwa mkoani Morogoro juzi.

Wabunge waliopata ajali na majimbo yao katika mabano ni Haji Ameir Haji (Makunduchi), Khamis Ali Vuai (Mkwajuni), Bhagwanji Maganlal Meisuria (Chwaka), Makame Mashaka Foum (Kijini) na Juma Othman Hija (Tumbatu).

Baada ya ajali hiyo, wabunge hao walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kabla ya jana mchana kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH).

Akitoa sababu ya kuwahamishia wabunge hao Muhimbili, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Morogoro, Dk Ritha Lyamuya alisema ni kwa ajili ya kupata vipimo zaidi ambavyo vingine havipatikani katika hospitali hiyo.

Baada ya rufaa hiyo, wabunge hao walisafirishwa kwa ndege mbili ndogo za kukodi za kampuni ya Safari Air Link.

Dk Lyamuya alieleza hali za wabunge hao kuwa wengi wamepata majeraha madogomadogo isipokuwa Mbunge wa Jimbo la Makunduchi, Haji Ameir Haji, ambaye amepata majeraha makubwa kichwani na kuvunjika mkono.

“Tulilazimika kumuweka Haji kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kutokana na majeraha na hali yake aliyokuwa nayo,” alisema Dk Lyamuya.

Ofisa uhusiano wa hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), John Masawe amethibitisha kupokewa kwa majeruhi hao.

Alisema waliwapokea wabunge hao jana saa saba mchana.

Masawe alisema majeruhi wote wapo chini ya uangalizi wa madaktari na hali zao zinaendelea vizuri.

“Miongoni mwao wapo walioumia mikono, vifua na mmoja ameumia kichwani, lakini Haji Ameir Haji aliumia zaidi kichwani na anaendelea na matibabu,” alisema.

“Huyu ameumia eneo la kichwani ila anaendelea vizuri na vipimo vya CT Scan vimechukuliwa kwa ajili ya matibabu zaidi,”alisema.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema ilitokea juzi saa tatu usiku, eneo la Gwata Maseyu barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya dereva wa gari hilo aina ya Prado kutaka kumkwepa mbwa, hivyo kuserereka na kupinduka.

Katibu wa Bunge, Steven Kigaigai alisema ameshapata taarifa za ajali ya wabunge hao sita na kwamba tayari kuanzia jana ofisi yake ilishaanza kuwashughulikia kwa kuwapa msaada wa kitabibu.

Kigaigai alisema mara baada ya kupokea taarifa hizo walifanya mawasiliano na uongozi wa hospitali ya Morogoro na walishauriwa kuwawahisha katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Ndiyo taarifa hizo ninazo, wamepata ajali huko Morogoro, tayari tumeshafanya taratibu za kuwapeleka Muhimbili kwa huduma zaidi na ofisi yetu inawajibika kwa kila hatua,” alisema Kigaigai

Wabunge wawaombea wenzao

Kufuatia ajali hiyo, wabunge wa Bunge la Muungano jana walizungumza na kuomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka.

Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly alisema, “Ajali ni popote, lakini kikubwa ni kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili awaponye haraka na warudi kutekeleza majukumu yao.”

Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha alisema ingawa ajali ni jambo la kawaida, idadi kubwa ya wabunge kupata ajali kwa wakati mmoja ni jambo linalotokana na ukata walionao wabunge.

Msabaha alisema maslahi ya wabunge ni kidogo ndiyo maana wanasafiri kwa wakati mmoja badala ya kutumia magari yao binafsi.

Mbunge wa Igunga, Dk Dalali Kafumu alisema, “Tuko pamoja nao, namuomba sana Mwenyezi Mungu awaponye haraka ili waje kuendelea na majukumu yao katika kipindi hiki cha bajeti, wawe na moyo wa subira kwani Mungu atasimama na mkono wake utakuwa pamoja nao.”

Imeandikwa na Hamida Sharif, Morogoro, Habel Chidawali, Dodoma na Elizabeth Edward, Dar es Salaam.