Waziri Mkuu awasili, ibada ya mazishi yaanza

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasili  katika viwanja vya Shule ya Sekondari Bwisya ambako inafanyika ibada ya mazishi ya watu waliokufa katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere

Ukerewe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasili  katika viwanja vya Shule ya Sekondari Bwisya ambako inafanyika ibada ya mazishi ya watu waliokufa katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere.

Akizungumza mapema asubuhi ya leo Septemba 23, 2018 mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema watakaozikwa katika makuburi hayo ni wale ambao hawajatambuliwa pamoja na waliotambuliwa lakini ndugu wameomba wazikwe kwenye makaburi yaliyoandaliwa na Serikali.

Kabla ya kuwasili kwa helkopta iliyombeba, Waziri Mkuu, ilitangulia helkopta nyingine ya polisi ambayo pamoja na ile ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) imekuwa ikifanya kazi ya kusomba dawa na vifaa tiba kutoka jijini Mwanza kwenda Kisiwa cha Ukara.

 

Waziri Mkuu amepokewa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama.

Tayari miili ya baadhi ya waliokufa katika ajali hiyo imewasili katika eneo la makaburi yaliyochimbwa hatua chache kutoka kilipozama kivuko hicho.