Wema apandishwa kizimbani kwa mara ya tatu

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtaka Miss Tanzania wa mwaka 2006, Wema Sepetu kutoweka video zinazohusiana na ngono wala maneno yoyote yenye mwelekeo huo katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram

 

Dar es Salaam. Wema Sepetu amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akishitakiwa kwa kosa la kusambaza video ya ngono katika mtandao wake wa Instagram.

Hii ni mara ya tatu kwa Wema kushtakiwa mahakamani. Februari, mwaka jana alifikishwa katika Mahakama ya Kisutu baada ya kukutwa na misokoto na vipisi vya bangi nyumbani kwake Kunduchi Ununio jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo alinusurika kwenda jela baada ya kulipa faini ya Sh2 milioni Julai 21 baada ya kutolewa hukumu na mahakama hiyo.

Hilo lilimtokea baada ya kutajwa kuwa mmoja wa watu wanaotumia dawa za kulevya katika orodha iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Mwaka 2013, Wema ambaye pia ni msanii wa filamu, alifikishwa katika mahakama ya Kinondoni kwa kosa la kuvunja kioo cha gari la Steven Kanumba, kilichokuwa na thamani ya Sh1 milioni.

Jana, baada ya kumsomea shitaka lake mbele ya Hakimu Maira Kasonde, Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombako aliiomba mahakama kumpatia masharti magumu ya dhamana Wema ili iwe fundisho kwa wengine kwa kuwa ni msanii mwenye wafuasi wengi wanaomuangalia hususan watoto.

Naye Ruben Simwanza, wakili wa Wema aliomba mteja wake apewe dhamana ya masharti nafuu kwa kuwa ni haki yake.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Kasonde alimtaka Wema kuwa na mdhamini mmoja ambaye angesaini bondi ya Sh10 milioni.

Wema alifanikiwa kukamilisha masharti ya dhamana na kuachiwa huru.

Baada ya kusikiliza hoja za pande hizo mbili, Hakimu Kasonde alimtaka Wema kuwa na mdhamini mmoja anayesaini bondi ya Sh10 milioni.

Wema alifanikiwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru.