Tanzania iweke mikakati kunufaika na uchumi wa buluu

Thursday February 14 2019Profesa Honest Ngowi

Profesa Honest Ngowi 

By Honest Ngowi

Kumekuwa na dhana mbalimbali katika maendeleo ya ya uchumi ikiwamo inayoibukia miaka ya hivi karibuni ya uchumi wa buluu.

Dhana hii inahusu shughuli za uzalishaji na utumiaji wa bidhaa na huduma baharini na maeneo yanayopakana na bahari kama vile fukwe. Dhana hii pia hujulikana kama uchumi wa bahari.

Ni dhana ambayo bado haijazungumziwa na kujadiliwa vya kutosha katika nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania licha ufukwe mrefu na sehemu kubwa ya bahari inayofaa kwa shughuli mbalimbali.

Jambo moja la uhakika ni kwamba, endapo dhana hii itatekelezwa vizuri inaweza kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi nchini itakayoongeza kipato cha wananchi pamoja na la Taifa kwa ujumla kw akutoa ajira mpya na kukuza uwekezaji.

Hamna maana moja inayokublika na kila mtu kuhusu uchumi wa buluu kwani taasisi na watu mbalimbali wametoa maana zao kuhusu dhana ya uchumi wa bahari.

Kimsingi maana zote zinaendana na hugusia mambo mengi yanayoshahabiana. Uchumi wa buluu unahusu matumizi na uhifahi wa rasilimali zinazopatikana baharini.

Benki ya Dunia inaelezea uchumi wa buluu kama utumiaji endelevu wa rasilimali za bahari kwa ajili ya ukuaji wa uchumi, kuboresha maisha na ajira na wakati huohuo kutunza mazingira ya bahari.

Umoja wa Ulaya unaelezea uchumi wa buluu kuwa ni shughuli zinazoendana na bahari na pwani katika sekta nyingi zilizofungamana na zinazoibukia. Jumuiya ya Madola inaona uchumi wa buluu kama dhana inayoibukia inayohamasisha matumizi na ulinzi bora wa rasilimali za bahari.

Wapo pia wanaoona uchumi wa buluu kuwa ni pamoja na faida za kiuchumi kutoka baharini kama vile utunzaji wa hewa ya ukaa, ulinzi wa fukwe, biyoanuwai na kadhalika.

Unahusu mchango wa bahari katika uchumi kwa ujumla wake, haja ya kushughulikia uendelevu wa mazingira na ikolojia ya bahari. Ni fursa ya ukuaji uchumi kwa nchi zinazoendekea na zilizoendelea.

Uchumi wa bahari

Wapo wanaochukulia dhana ya uchumi wa buluu kuwa sawa na uchumi wa bahari. Hata hivyo kuna tofauti za msingi kati ya dhana hizi. Dhana ya uchumi wa bahari ni finyu na ndogo kuliko ile ya uchumi wa buluu.

Dhana hii inajishughulisha na matumizi ya rasilimali za bahari tu lakini ile ya uchumi wa buluu ni dhana pana zaidi. Haijikiti katika kuona bahari kama fursa ya ukuaji uchumi bali unatizama masuala ya kiikolojia.

Dhana ya uchumi wa buluu inaweza jina jipya. Hata hivyo sio mpya kwa maana pana ya yanayofanyika katika uchumi huu. Kinachofanywa na dhana hii ni kutoa jina kwa mambo ambayo kimsingi yamekuwa yakifanyika ndani ya bahari zetu na pwani zake kwa muda mrefu.

Shughuli hizi ni pamoja na uvuvi wa aina mbalimbali ukiwemo wa kibiashara na usio wa kibiashara katika kina kirefu na kifupi. Nyingine ni shughuli za usafrishaji kama vile kwa kutumia meli na mitumbwi, shughuli za utafutaji na uchimbaji madini na mafuta baharini, shughuli za starehe kama michezo na hoteli za kandokando mwa bahari na shughuli za bandari katika upana wake.

Masuala mengine ni ujenzi wa vyombo vya baharini kama vile meli na shughuli za elimu na utafiti kuhusu mambo ya bahari. Zote hizi ni shughuli za uchumi wa buluu.

Kinachoziweka pamoja shughuli hizi ni bahari ambayo inakuwa jukwaa ambalo juu, ndani, chini hata kando yake shughuli hizi zinafanyika.

Ushauri

Ni vizuri kuiona dhana ya uchumi wa buluu kama fursa kwa ajili ya fikra na mabadiliko ya kiuchumi. Zipo nchi mbalimbali zilizojikita katika uchumi wa buluu kama jukwaa la kujikomboa na kujiendeleza kiuchumi.

Kati ya nchi hizi ni zile za umoja wa nchi ishirini zinazooshwa na Bahari ya Hindi ikiwemo Tanzania. Umoja huu unaitwa Indian Ocean Rim Association (IORA). Mwandishi wa makala haya ni mdau wa umoja huu kupitia jukwaa la wanataaluma.

Uchumi wa buluu ni kati ya maeneo yanayoangaliwa kwa jicho la kipekee katika umoja huu. Kwa Afrika, ni Afrika Kusini tu iliyo mbele zaidi katika kuendeleza na kutumia dhana ya uchumi wa buluu kama mkakati wake wa maendeleo ya uchumi.

Ni vizuri kwa Tanzania kujifunza namna ambavyo nchi nyingine zinavyotumia dhana hii kama fursa ya uchumi si kwa mtu mmoja mmoja tu bali kwa Taifa kwa ujumla.

Advertisement