Kampuni zateketeza dawa za Sh92 milioni

Friday October 23 2015

 

By Hawa Mathias, Mwananchi

Mbeya. Kampuni tatu za maduka ya dawa za binadamu mkoani Mbeya zimeteketeza dawa zilizokwisha muda wake zenye thamani ya Sh92 milioni baada ya kuzipeleka kwenye Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Mkaguzi wa Dawa wa TFDA Mkoa wa Mbeya, Dk Silvester Mwidunda alisema jana kuwa kampuni hizo ziliwajibika zenyewe kukusanya dawa hizo na kuziwasilisha kwao ili ziteketezwe.

Dk Mwidunda alisema kwa mujibu wa Sheria ya Dawa ya Mwaka 2003 kila mfanyabiashara wa maduka ya dawa na vipodozi anapaswa kusalimisha bidhaa zilizokwisha muda.

Alisema mbali na dawa, TFDA pia iliteketeza vipodozi vyenye thamani ya zaidi ya Sh8 milioni vilivyokamatwa katika maduka mbalimbali jijini hapa.

Mkaguzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini , Yusto Wallace alisema kuna changamoto kubwa ya uingizwaji holela wa dawa na vipodozi hali inayochangiwa na ushirikiano hafifu katika mipaka ya Malawi na Zambia.

Alisema kutokana na changamoto hiyo wameweka mikakati ya kufanya mikutano ya ujirani ili kuona namna kutokomeza bidhaa hizo.

Advertisement

Mfanyabishara wa duka la madawa muhimu, Ditram Kutemile alisema ili Serikali iweze kufikia malengo ni lazima itoe elimu kwa wafanyabishara katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani.

Alisema hiyo itasaidia kupunguza utitiri wa dawa na vipodozi bandia au vilivyokwisha muda wake kuingizwa kwenye soko.

Advertisement