Harry, Meghan wanavyoivuruga familia ya kifalme Uingereza

Unaweza kusema kuwa mwanamfalme Harry na mkewe Meghan wameanza mwaka 2020 kwa uamuzi wa kuishangaza dunia.

Hatua hiyo inatokana na kutangaza kwamba wanataka kuachana na majukumu yao ya ngazi za juu katika familia ya kifalme na kuamua kuishi maisha ya kawaida.

Hatua hiyo imezua mjadala kwa zaidi ya wiki moja sasa, kiasi cha kulifunika sakata la Brexit lililotikisa katika miezi ya hivi karibuni nchini humo.

Uamuzi huo unatajwa kuwa ni wa kwanza kutokea katika himaya ya ufalme na baadhi ya Waingereza wanaona jambo hilo si la kawaida.

Uamuzi huo wameupa jina maarufu la Megxit ikiwa kama kashfa juu ya Meghan anayelaumiwa kumshawishi Harry kuridhia kitendo hicho cha kujitoa.

Wanandoa hao wamesema wanapanga kutumia muda wao mwingi Amerika ya Kaskazini. Pia wanataka kujitegemea kifedha badala ya kutegemea mapato yatokanayo na nafasi zao za kifalme.

Kutokana na uamuzi huo, sasa maisha ya wanandoa hao yatakuwa katika nchi mbili za Canada na Uingereza katika kipindi cha mpito, wakati mchakato wa kujitoa ukiendelea.

“Tumeamua kufanya mabadiliko mwaka huu kwa kuanza kutekeleza jukumu jipya ndani ya taasisi hii,” alisema Harry ambaye yuko nafasi ya sita katika orodha ya warithi wa kiti cha Ufalme.

Wamesema watawasilisha maelezo kamili juu ya hatua yao, wakati wakijadiliana na Malkia Elizabeth, baba yake Harry, mwanamfalme Charles na William ambaye ni kaka yake.

Uamuzi huo ulionekana kuwashangaza wanafamilia wa kifalme akiwamo Malkia, kwani haukuwa ukifahamika. Malkia Elizabeth ametaka suala hilo lijadiliwe hasa kuhusu usalama wao.

Wanandoa hao walifikia uamuzi huo bila kumshirikisha Malkia wala mwanamfalme William na waandamizi wengine katika familia hiyo ya kifalme, ingawa wanasema walifikiria uamuzi huo kwa muda mrefu na kufanya uamuzi huo miezi mingi iliyopita.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala la kifalme Uingereza wamebeza hatua hiyo wakisema inakiuka taratibu kadhaa za namna ya kuishi kama wana wa mfalme au wanaotoka ukoo wa kifalme.

Kabla ya kufikia uamuzi huo Oktoba mwaka jana wanandoa hao walilalamika kuingiliwa maisha yao kwa kufuatwa na vyombo ya habari kwa kivuli cha kutoka familia ya kifalme.

Harry (35) na Meghan (38) walioana mwaka 2018 katika sherehe zilizofanyika kwenye kasri la Windsor. Mei 6, 2019 walipata mtoto wao wa kwanza wa kiume.

Harry ameonyesha wasiwasi kwamba huenda mkewe akakutana na yaliyomkuta mama yake, Princess Diana na kusababisha kifo chake.

Je uamuzi wa wanandoa hao una maana gani kwa familia ya kifalme? Wataendelea kuwa salama wakiwa nje ya Uingereza? Nani atagharamia ulinzi wa mwanamfalme huyo?

Haya ni baadhi ya maswali ambayo wanafamilia na watu wengine wanajiuliza.

Malkia akubali

Katika kikao kilichofanyika mwanzoni mwa wiki hii, Malkia Elizabeth II (93) amekubali kuwapo kipindi cha mpito wakati mwanamfalme Harry na mkewe watakuwa wakiishi Canada na Uingereza.

Malkia huyo alisema anaamini uamuzi wa mwisho kuhusu hilo utafanyika hivi karibuni.

Alisema Harry na mkewe bado ni watoto wa kifalme na wataendelea kuthaminiwa wakati wanaendelea kujitegemea.

Waziri Mkuu Canada

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau alisema mazungumzo zaidi yanahitajika kuhusu gharama za usalama na mipango mingine kuhusu Harry na Meghan.

Akizungumza katika kipindi cha Global News, kupitia Shirika la Utangazaji la Canada, Trudeau alisema raia wengi wa Canada wanaunga mkono hatua hiyo, ingawa bado kuna umuhimu wa majadiliano zaidi kwa kuwa Serikali ya Canada haijahusishwa kuhusu kitakachohitajika katika hatua ya wanandoa hao kuishi nchini humo.

Kifo cha mama yake

Harry ni mmoja wa wahanga wa ufuatiliaji wa kukithiri wa vyombo vya habari, kwani mama yake, marehemu Princess Diana alifuatiliwa mpaka akafa katika ajali akiwa anawakimbia waandishi wa habari mwaka 1997.

Diana alifariki dunia Agosti 31 akiwa na miaka 36, baada ya gari alilokuwamo akisafiri pamoja na mpenzi wake Dodi al Fayed kupata ajali kwenye njia ya chini kwa chini mjini Paris, Ufaransa.

Wakati anafariki dunia, watoto wake William na Harry walikuwa na umri wa miaka 15 na 12.

Meghan mke wa Harry

Mke wa mwanamfalme Harry, Meghan alikuwa muigizaji nchini Marekani na moja kati ya kazi zake maarufu ni kucheza nafasi ya mwanasheria katika tamthilia ya “Suits”.

Meghan, raia wa Marekani aliwahi kuolewa na muongozaji wa filamu, Trevor Engelson mwaka 2011 na kuachana mwaka 2013.

Mke huyo wa Harry alipata kuwa balozi wa Shirika la World Vision na aliwahi kwenda Rwanda kuhamasisha upatikanaji maji na kuwatembelea Wamarekani wanaolinda amani Afghanistan.

Pia amewahi kutembelea nchi mbalimbali kuhamasisha haki za msichana anapokuwa katika hedhi.

Mtawala wa sasa Uingereza

Malkia Elizabeth II ndiye mtawala anayeongoza sasa akiwa ameshika madaraka hayo tangu mwaka 1952 baada ya kifo cha baba yake Mfalme George VI.

Malkia Elizabeth aliyezaliwa Aprili 21, 1926, alizaa watoto wanne akiwamo mwanamfalme Charles ambaye alipomuoa Diana Spencer walipata watoto wawili; William na Harry kabla ya kuachana mwaka 1996.

Katika kurithi nafasi ya Malkia Elizabeth II, kwa sasa kuna orodha ya watu saba ambao ni Charles akifuatia mwanaye William na watoto wake watatu ambao ni George, Charlotte na Louis. Anayefuata katika orodha hiyo ni Harry.

Vyanzo vya mapato

Vipo vyanzo vitatu vya mapato ya ukoo wa kifalme, kwanza ni ruzuku kutoka Serikali Kuu, kodi kutoka serikali nyingine za Uingereza na tatu ni utajiri wa Malkia na vyanzo vyake vya mapato.

Makala kwa msaada wa mitandao