Hesabu tatu zaitesa Marekani kuivamia Iran, Korea Kaskazini

Saturday January 11 2020

 

By Luqman Maloto, Mwananchi

Dunia ilitarajia Jumatano iliyopita, Marekani ingetangaza vita dhidi ya Iran. Badala yake, Rais Donald Trump alitoa vitisho na kuahidi kuongeza vikwazo vya kiuchumi kwa nchi hiyo.

Kwa ile hotuba ya Trump, watu wanasema Marekani imeufyata. Hupaswi kuamini hivyo, Wamarekani hawaufyati. Ukiona Marekani inaingia vitani leo, ujue ina uhakika wa kushinda bila yenyewe kupata madhara. Hiyo ndiyo falsafa yao.

Marekani ina uzoefu wa vita kwa faida na kwa hasara. Ilijijenga sana kiuchumi wakati wa Vita Kuu vya Pili vya Dunia. Iliathirika sana kiuchumi kupitia Vita vya Vietnam, Korea, vilevile dhidi ya Saddam Hussein, Iraq.

Wamarekani wanayajua maumivu ya kupigwa vitani. Jinsi jeshi la Cuba lilivyoidhalilisha Marekani katika vita ya Bay of Pigs Invasion. Kikosi kilichotengenezwa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), kilichoitwa Brigedi 2506, kilichoingia Cuba kumpindua aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Fidel Castro, kilidhibitiwa Aprili 17, 1961.

Wanajeshi wa Marekani walilazimishwa kusalimu amri ndani ya siku tatu tangu kuanza kwa mapigano. Hakuna wakati mbaya Marekani ilijiona imedhalilishwa vitani kama hapo.

Vita ya Korea

Advertisement

Korea lilikuwa taifa moja kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Na ilikuwa koloni la Japan. Baada ya Japan kudhoofishwa na pigo la nyuklia , lililopigwa na Marekani katika miji ya Nagasaki na Hiroshima, Korea iligawanywa.

Marekani walichukua Kusini na Urusi Kaskazini. Na hiyo ndiyo ikawa sababu ya kuundwa kwa nchi mbili, Korea Kaskazini na Korea Kusini.

Mwanzo wa Vita ya Korea ni Marekani kuitangaza Korea Kaskazini kuwa iliivamia Korea Kusini, hivyo mapambano yalianza. Awali, ilionekana kama Marekani isingetumia msuli mkubwa kuikabili Korea Kaskazini.

Hata hivyo, Marekani ikiwa imeweka kambi ya vita ambayo hufahamika kama Chosin Reservoir Campaign, Novemba 27, 1950 ilishambuliwa kwa kushtukizwa na China, hivyo mapigano makali yalitokea.

China iliamua kuishambulia Marekani ili kudhoofisha mpango wake wa kuipiga Korea Kaskazini. Mapambano hayo ambayo yalidumu kwa siku 16 kati ya China na Marekani, huitwa Battle of Chosin Reservoir. Yalianza Novemba 27 mpaka Desemba 13, 1950.

Vita ya Vietnam na Saddam

Mwaka 1955 Marekani waliamua kujitosa kwenye Vita ya Vietnam, iliyokuwa inahusisha makundi ya itikadi hasimu, ubepari na ukomunisti.

Marekani waliingia kusaidia kundi lililokuwa na mrengo wa ubepari. Moto uliowaka haukuwa mdogo. Vita ilipiganwa miaka 20 mfululizo. Hasara ambayo Marekani iliipata haiwezi kufidiwa. Hakuna ushindi uliopatikana.

Agosti 2, 1990, Marekani ikiungwa mkono na mataifa 35 duniani, ilifungua mashambulizi dhidi ya Iraq ya Saddam Hussein. Ilikuwa baada ya Saddam kuivamia Kuwait na kusababisha mgogoro wa mafuta duniani.

Pamoja na kwamba Marekani ilifanikiwa kuikomboa Kuwait kutoka kwenye himaya ya Saddam, nguvu iliyotumika ilikuwa kubwa lakini matokeo hayakuwa rahisi. Mataifa 35 dhidi ya moja, lakini vita ilidumu miezi sita.

Dhamira ya Marekani kumwondoa Saddam madarakani iliendelea kwa zaidi ya muongo mmoja. Iraq ilisulubiwa kwa vikwazo vya kiuchumi. Siku Marekani ilipojiridhisha kuwa Saddam hana nguvu tena, ikawa sababu ya uvamizi wa mwaka 2003, wakamng’oa. Saddam akanyongwa.

Marekani walijiridhishaje kuwa Saddam hana nguvu? Jibu ni kujidanganya kwa Saddam. Aliamini Marekani walikuwa tayari kwa maridhiano, hivyo akaruhusu wakaguzi wa Kimarekani waingie nchini kwake wajiridhishe kwamba hakuwa akimiliki silaha za sumu.

Wakaguzi waliporudisha majibu kuwa Iraq haikuwa na silaha za maangamizi, badala ya Marekani kupongeza, ndio kwanza waliivamia bila hata kufanya mashauriano na Umoja wa Mataifa.

Ni kwa sababu Marekani kuipigia kelele Iraq kuwa ilikuwa na silaha za sumu, ilikuwa propaganda kutaka kujua ilikuwa na nini. Je, ilikuwa na nguvu kama za mwaka 1990 mpaka 1991 au ingepigika kwa urahisi? Walipogundua inapigika, wakaivamia Iraq kipindi ambacho dunia nzima ililaani.

Iran ni hesabu tu

Ingekuwa amri ya Trump na jazba zake, Jumatano iliyopita vita ingetangazwa. Tatizo, majenerali wa Marekani wanatambua hesabu za kuipiga Iran hazijakaa sawa.

Hesabu ya kwanza ni nguvu ya Iran kijeshi. Wana silaha za aina gani? Zinaweza kusababisha madhara makubwa kiasi gani?

Kumbukumbu ya Vita ya Vietnam, Korea, Bay of Pigs na nyingine ambazo Marekani ilipata wakati mgumu ndiyo inayolifanya taifa hilo litafute hesabu za kuivamia Iran.

Iran wana silaha gani na wapo na nani? Yasije kutokea ya mwaka 1950, wanajipanga kuipiga Korea Kaskazini, wakajikuta wanapigwa na China kisha Urusi.

Hesabu hii ndiyo iliwapa ushindi kwa Saddam, walimkagua na kugundua hana kitu na kumwondoa. Wamarekani hawajapata fursa ya kuikagua Iran. Wairan hawajatoa huo mwanya.

Hesabu hiyohiyo ndio inafanya Korea Kaskazini ibaki salama leo. Mwaka 2017, Marekani walipeleka meli yao ya kivita na vifaa vyao mpaka kwenye peninsula ya Korea Kaskazini, lakini hawakuishambulia.

Ni kwa sababu Marekani hawajui siri ya silaha ndani ya Korea Kaskazini.

Hesabu ya pili ambayo Marekani wanacheza nayo ni madhara. Je, wataweza kuipiga Iran bila wao kupata madhara? Na wakipigana madhara yatakuwa kiasi gani? Vifo, majeruhi na uharibifu wa vifaa.

Siku wakipiga hesabu na kuona uwiano wa madhara ni chanya kwao, ni hakika wataipiga Iran. Hata Korea Kaskazini. Ni hesabu tu. Zingatia Wamarekani huogopa kufa, halafu Waajemi (Iran) wanaamini kifo ni lifti ya peponi.

Kifo chochote ni ushindi, wakimuua Mmarekani wanaamini wamemuua kafiri (ushindi), wakiuawa wanaamini wamekufa shahidi, hivyo wanakwenda peponi. Marekani kifo ni hasara. Hamasa ya kupigana haipo sawa.

Hesabu ya tatu ni jinsi ya kumaliza vita. Afghanistan waliwaondoa Taliban lakini mpaka leo vita haijaisha. Iraq moto unaendelea. Libya tangu mwaka 2011 mpaka leo damu inamwagika. Sasa iongezeke na Iran yenye Waajemi wenye historia ya kupigana kwa roho na mwili pasipo kuogopa silaha.

Malengo ya kufanya uvamizi yalitimia Iraq, Saddam aling’oka, Afghanistan, Taliban walipinduliwa ambao ndio walimhifadhi Osama bin Laden. Libya, Muammar Gaddafi aliondoshwa na kuuawa. Tatizo baada ya hapo, vita vimeshamiri na mataifa hayo yamegeuka himaya ya ugaidi na uhalifu wa kumwaga damu kuliko ilivyokuwa kabla.

Ongeza na Syria, uvamizi wa Marekani kuuondoa utawala wa Bashar al Assad, umesababisha nchi hiyo igeuke maskani ya ugaidi.

Hizo ndiyo hesabu ambazo zinaifanya Marekani isite kuivamia Iran wala Korea Kaskazini. Siku zikikaa sawa, vita itachukua nafasi. Tamko la Marekani kutaka amani si la kweli, maana waliivamia Iraq kipindi haikuwa na silaha za sumu wala za masafa marefu. Walimpiga Saddam kipindi ambacho alikuwa ameamua kustawisha amani. Walimtwanga Gaddafi akiwa hana madhara yoyote kwa dunia.

Advertisement