Maandalizi vifaatiba vya corona yaanza

Muktasari:

Kwa mujibu wa Unicef, itahifadhi mabomba milioni 520 ya sindano kwenye bohari zake ili kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka 2021 iwe na mabomba bilioni 1.

Geneva. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), limeanza maandalizi ya kuhakikisha mabomba ya sindano ya chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 yanatolewa na kusambazwa mapema.

Taarifa ya Unicef iliyotolewa jijini New York, Marekani inasema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa dunia itahitaji mabomba mengi ya sindano sambamba na dozi zenyewe.

Kwa mujibu wa Unicef, itahifadhi mabomba milioni 520 ya sindano kwenye bohari zake ili kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka 2021 iwe na mabomba bilioni 1.

Mkurugenzi mtendaji wa Unicef , Henrietta Fore alisema: “Tutahitaji kufanya kazi kwa haraka kadri chanjo hiyo inavyotengenezwa. Ili kwenda haraka, tunalazimika kuanza kazi hiyo sasa. Mwishoni mwa mwaka huu, tutakuwa tayari tuna mabomba nusu milioni ya kutolea chanjo yakiwa yamehifadhiwa, yatasambazwa haraka na kwa gharama nafuu.”

Kila kasha moja linachukua mabomba na sindano 100 na kwamba makasha hayo yanaweza kuhifadhiwa kabla ya matumizi kwa miaka mitano.

Shirika hilo linasema kwa upande wa chanjo ili kuhakikisha inasafirishwa salama na katika kiwango cha joto kinachotakiwa, tayari kwa kushirikiana na Shirika la Afya la Duniani (WHO), wanapanga mpango wa kupata mifumo ya usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa kwa ubaridi kwa ubia na sekta ya umma na binafsi.