Musharraf apinga hukumu ya kifo akiwa kitandani uhamishoni

Rais wa zamani wa Pakistan, Pervez Musharraf

Muktasari:

Asema mashtaka na hukumu hiyo vimetokana na chiki binafsi

Islamabad. Rais wa zamani wa Pakistan, Pervez Musharraf amesema kutiwa kwake hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo vimetokana na chuki binafsi.

Uamuzi huo wa mahakama maalumu, umeweka rekodi kwa mtu aliyewahi kuwa kiongozi wa nchi hiyo kutiwa hatiani na kuhukumiwa kifo kwa makosa ya uhaini, katika nchi ambayo jeshi limekuwa na madaraka makubwa kwa karibu nusu ya umri wake.

“Hii kesi ilifunguliwa na kuendeshwa kwa chuki binafsi dhidi yangu,” alisema Musharraf katika mkanda wa video uliorekodiwa juzi Jumatano usiku.

Musharraf – anayeaminika kuwa uhamishoni Dubai ambako pia afya yake inatetereka, alionekana katika kitanda cha hospitali akiwa dhaifu na akiongea kwa taabu.

Hata hivyo, jenerali huyo wa zamani alisema hajaamua hatua inayofuata, wala iwapo wanasheria wake wanapanga kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Kesi ya uhaini dhidi yake iliyoanza mwaka 2013, inahusu uamuzi wake wa kusimamisha Katiba na kutangaza utawala wa dharura mwaka 2007.

Hukumu hiyo imezikasirisha mamlaka za usalama za Pakistan, na msemaji wa jeshi amelaani uamuzi huo akisema umeyaumiza na kuyasikitisha majeshi ya ulinzi.

“Mkuu wa zamani wa majeshi, mwenyekiti wa kamati ya wanadhimu na Rais wa Pakistan ambaye ametumikia nchi kwa zaidi ya miaka 40, amepigana vita kuilinda nchi, hawezi kamwe kuwa msaliti,” jeshi la Pakistan lilisema Jumanne.

Waziri mkuu Imran Khan, mpinzani wa zamani wa Musharraf hajasema lolote kuhusu hukumu hiyo.

Khan anaaminika kuwa karibu na jeshi na mawaziri wake wengi wamewahi kufanya kazi na Musharraf katika serikali ya kijeshi.