Aliyepona corona sasa achangia kingamwili

Akiwa anatoka katika karantini, baada ya ku pona Covid-19, Diana Berrent ana hamu ya kuingia katika vita dhidi ya ugonjwa huo wa virusi vya corona na amejitolea kingamwili ambazo watafiti wana imani zitasaidia wengine.

Katikati ya mwezi Machi, mkazi huyo wa New York aliamka huku mwili ukiwa na joto la nyuzi 39 na kikohozi, na kuwa mmoja wa watu wa kwanza kugundulika kuwa na virusi vya corona katika kisiwa cha Long.

Wiki hii, Berrent amekuwa mtu wa kwanza kupona ugonjwa huo katika jimbo lake ambaye alichunguzwa kingamwili protini katika mfumo wa kinga ambazo zinaweza kupambana na virusi kwa ajili ya kuchangia majaribio ya mwanzo ya matibabu ya maambukizi hayo ambayo yameshaua zaidi ya watu 51,000 duniani kote.

Convalescent plasma, majimaji yaliyo katika damu pamoja na kingamwili zilizomo mwilini baada ya mtu kuugua, zimeonyesha kuwa na ufanisi kutibu magonjwa yanayoambukiza kama Ebola na SARS.

Kwa sasa, Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani imetoa ruhusa kwa madaktari kujaribu mkakati huo wakati wagonjwa wa virusi vya corona wakijaa hospitalini huku watu walioambukizwa nchini Marekani wakizidi 245,000.

Bruce Sachias, mganga mkuu wa kituo cha damu cha New York ambacho kitakusanya, kujaribu na kusambaza michango katika jiji hilo, alisema kuna sababu ya kuamini kuwa uongezaji wa plasma unaweza kusaidia kuondoa tatizo la sasa, majaribio yanaendelea hayalengi kuzaa suluhisho kamilifu.

“Ni muhimu sana kwetu kujua kuwa bado tuko katika mazingira mapya kabisa,” alisema.