Bilionea Kenya kortini kwa tuhuma za kukwepa kodi

Muktasari:

Jumatano iliyopita Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma nchini Kenya (DPP), Noordin Haji aliagiza kukamatwa kwa bilionea Humphrey Kariuki kwa tuhuma za kukwepa kodi.

Nairobi, Kenya. Mfanyabiashara na bilionea, Humphrey Kariuki amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kukwepa kodi ya Sh17 bilioni karibu Sh374 bilioni za Kitanzania.

Bilionea Kariuki pamoja na washtakiwa wengine wanane wamefikishwa katika Mahakama Kuu ya Kenya leo Jumatatu Agosti 19 wakikabiliwa na mashtaka tisa.

Kariuki alifikishwa mahamani hapo kufuatia amri ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma nchini Kenya (DPP), Noordin Haji kuagiza mfanyabishara huyo kukamatwa kwa kwa tuhuma za kukwepa kodi ya Sh41 bilioni karibu Sh1 trilioni kupitia kiwanda chake cha vinywaji vikali cha Thika.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni wakurugenzi wa kiwanda cha vinywaji vikali cha Thika, Stuart Gerald Herd, Robert Thinji Muriithi, Njenga Kuria na Geoffrey Kaaria Kinoti Mbombua.

Aidha, watuhumiwa wao wengine wanakabiliwa na mashtaka 21 ya ukwepaji kodi na kuwa na stakabadhi bandia.

Mara baada ya kusomewa mashtaka hayo, wakili wa bilionea huyo, Kioko Kilukumi aliiomba mahama kumpatia dhamana mteja wake ili aweze kuendelea na shughuli zake kwa kuwa ni mwekezaji.

Wakili huyo pia aliiomba mahakama hiyo kutoishikilia paspoti za mteja wake ikiwamo ya Kenya na Cyprus.

Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na upande wa mashtaka kwa madai kuwa ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) haijakamilisha upepelezi wa kesi hiyo.

Mwendesha mashtaka, Vincent Monda alidai kuwa upande wa mashtaka pia unahitaji kuangalia hati zake za kusafiria ili kuhakikisha hawezi kutoroka.

Kabla ya kukamatwa kwa bilionea huyo, Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA) ilifunga akaunti zake kumi na moja.