Chuo kikuu Kenyatta chafungwa muda usiojulikana

Muktasari:

Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini Kenya kimefungwa kwa muda usiojulikana baada ya wanafunzi kuandamana kwa siku mbili wakipinga mambo mbalimbali ikiwamo kutumia daraja la juu lililopo katika chuo hicho.

Kenya. Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini Kenya kimefungwa kwa muda usiojulikana baada ya wanafunzi kuandamana kwa siku mbili wakipinga mambo mbalimbali ikiwamo kutumia daraja la juu lililopo katika chuo hicho.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Oktoba 9, 2019 na makamu wa Chuo hicho Profesa Paul Wainana inaeleza kuwa seneti imefikia uamuzi huo kutokana na fujo zilizosababisha kutoendelea kwa masomo na uharibifu wa mali za chuo.

“Kwa yanayoendelea wanafunzi wote wanatakiwa kuondoka chuoni haraka iwezekanavyo,” imeeleza taarifa ya Wainana.

Hata hivyo, kiongozi wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Kenyatta (Kusa), Joshua Ayika amewataka wanafunzi kupuuza kauli ya Wainana  badala yake kusubiri taarifa atakayotoa.

Oktoba 7, 2019 wanafunzi hao waliibua mvutano na polisi kwenye maandamano yaliyoongozwa na Ayika wakishinikiza Wainana ajiuzulu hali iliyosababisha foleni katika barabara ya Thika.

Sababu nyingine ya maandamano hayo ni kutangazwa mapema kwa tarehe ya mwisho kulipa ada, kufukuzwa kwa wanafunzi na uongozi wa wanafunzi.

“Wafanyakazi wamekuwa wakifukuzwa bila kupewa taarifa rasmi, takribani wafanyakazi 700 wamefukuzwa kitu ambacho si cha kiungwana,” amesema Ayika.

Taarifa nyingine ya chuo hicho imeeleza Ayika alisambaza taarifa bila kuwashirikisha viongozi wenzake pia umeomba radhi kwa umma kufuatia baadhi ya wanafunzi kufanya maandamano badala ya kutumia njia ya mazungumzo na uongozi wa chuo.