Dunia yalaani shambulizi la Iran

Thursday January 9 2020

 

Dunia imeendelea kulaani mashambulizi ya Iran kwenye kambi inayotumiwa na Marekani nchini Iraq.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami (Nato), Jens Stoltenberg ameandika kwenye ukurasa wa Twitter akilaani tukio hilo na kutoa mwito wa kujizuia ili kuepusha machafuko zaidi.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Mje wa Ufaransa, Jean-Yves le Drian yeye ametaka kukatishwa kwa mzunguko wa machafuko na kusisitiza pande zote mbili kujizuia na kuwajibika tangu shambulizi la Marekani lililomuua Jenerali Qassemi Soleimani wa Iran, wiki iliyopita.

Naye Waziri mkuu wa Uingereza, Boris Johnson pia amelaani shambulizi hilo akiitaka Iran kutorudia mashambulizi ya kipuuzi na hatari, na badala yake watafute mbinu za dharura za kuzuia kuongezeka kwa mgogoro.

Hata Spika wa Bunge la Iraq, Mohammed al-Halbusi amelaani mashambulizi hayo ya Iran aliyoyataja ni ukiukwaji wa uhuru wa taifa hilo.

Lakini Rais wa Iran, Hassan Rouhani amelishukuru jeshi la walinzi wa amani kwa jibu hilo la kishujaa kwa Marekani.

Advertisement

Rais huyo wa Iran ameionya Marekani kufikiria mara mbili kabla haijalipiza kisasi cha shambulizi la Iran kwenye kambi ya Marekani iliyopo Iraq ambalo pia lilikuwa la kisasi dhidi ya mauaji ya Soleimani.

Rouhani amenukuliwa akisema iwapo Marekani inapanga mashambulizi na uhalifu dhidi ya Iran, watalipiza kisasi na mashambulizi makubwa zaidi.

Ameliita shambulizi dhidi ya Soleimani kuwa ni uhalifu wa kivita wa Marekani ambao umewaleta pamoja zaidi watu wa Iran.

Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump amesema nchi hiyo haitalipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi ya kijeshi bali kwa kuweka vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya Iran.

Advertisement