Heche akwamisha kesi ya vigogo Chadema

Muktasari:

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ambaye ni mmoja wa washtakiwa katika kesi ya uchochezi inayomkabili yeye na viongozi wengine wanane wa Chadema, katika Mahakama ya Kisutu, ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kuhudhuria matanga ya kaka yake na hivyo kusababisha mahakama hiyo kushindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, nchini Tanzania imekwama kuendelea na kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kutokana kutokuwepo mahakamani kwa mshtakiwa John Heche.

Mahakama hiyo ilipanga leo Jumatatu Agosti 5,2019 kutoa uamuzi wa kuoneshwa au kutokuoneshwa kwa mkanda wa video uliopokewa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka na kuendelea na usikilizwaji wa upande wa mashtaka.

Hata hivyo, kutokana na kutokuwepo kwa Heche ambaye ni mshtakiwa wa nane katika kesi hiyo, mahakama hiyo imeshindwa kuendelea na usikilizwaji huo wala utoaji wa uamuzi huo na badala yake imeahirisha kesi kwa muda wa siku kumi.

Kiongozi wa jopo la mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Peter Kibatala, ameieleza mahakama hiyo kuwa Heche ambaye ni Mbunge wa Tarime Vijijini, hakuweza kufika mahakamani kwa kuwa alifikiwa na kaka yake na bado anaendelea na matanga.

Ameifahamisha mahakama kuwa waliandika barua mahakamani kuelezea uwezekano wa Heche na Mbowe kutokuwepo kwa kuwa wote wamefiwa na kaka zao.

“Mheshimiwa hakimu, kama tulivyoeleza kwenye barua hiyo ambayo tumewapa nakala upande wa mashtaka, tulitarajia kwamba hata mshtakiwa wa kwanza, (Mbowe) asingekuwepo leo, lakini yeye ameweza kufika, ila Heche hakuweza kwani bado anaendelea na matanga. Hivyo tunaomba ahirisho hadi tarehe nyingine.”, amesema Wakili Kibatala.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi umeileza mahakama kuwa hauna pingamizi dhidi ya maombi hayo kutokana na kutokuwepo kwa mshtakiwa huyo, ila akaomba mahakama ipange tarehe nyingine ya karibuni kuendelea na kesi hiyo pia ipange muda mrefu.

“Kutokana na mazingira haya hatuna pingamizi lolote, ila tu tunaomba ipangiwe muda za wa kuendelea na usikilizwaji,” amesema Wakili Nchimbi na kuongeza:

“Bila kuingilia kalenda ya mahakama, tunaomba ipangiwe tarehe nyingine ya karibuni, kwani shahidi huyu tumemuweka kwa muda wa wiki mbili sasa na alipaswa kuwa Nairobi.”

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba anayeisikiliza kesi hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kurejea kusoma barua hiyo ya kuomba ahirisho, amekubaliana na maombi hayo.

Hivyo  amepanga kuendelea na kesi hiyo kwa kutoa uamuzi huo na kisha kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi kwa siku tano mfululizo, kuanzia Agosti 15 hadi 21, 2019.

Katika uamuzi huo, mahakama inatarajiwa kuamua iwapo itakubaliana na maombi ya upande wa mashtaka kutumia vifaa kutoka Kituo cha Habari na Mafunzo cha Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Lushoto, kilichoko Kisutu Dar es Salaam, kuonesha maudhui ya video hivyo.

Hata hivyo maombi hayo ya upande wa mashtaka kutumia kituo hicho na vifaa hivyo yalipingwa na wakili Kibatala akidai pamoja na mambo mengine kuhusu utaratibu uliotumiwa na upande wa mashtaka, akidai kuwa walipaswa kuiandikia mahakama barua kuomba maudhui ya video hiyo yaoneshwe.

Pia Wakili Kibatala alidai upande wa mashtaka ndio uliopaswa kuandaa vifaa vyote muhimu vya kuoneshea maudhui yaliyomo katika mkanda huo wa video.

Mbali na Mbowe na Heche, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Vigogo hao wa Chademea wanaokabiliwa na kesi hiyo ni  Katibu Mkuu, Dk Vicent  Mashinji, manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na mweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko, mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.

Washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12, ambayo ni kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali, yanayowakabiliwa washatakikwa wote, huku Mbowe, Msigwa Mdee na Heche kila mmoja peke yake akikabiliwa na mashitaka zaidi. 

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika Barabara ya Kawawa, Mkwajuni, Kinondoni na kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.

Mbowe peke yake anakabiliwa na mashtaka matano ya kuhamasisha chuki kwa jamii dhidi ya Serikali, uchochezi na uchochezi wa uasi na ushawishi wa kutenda kosa.

Msigwa peke yake anakabiliwa na shtaka la ushawishi wa kutenda kosa, akidaiwa kuwashawishi wakazi wa wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, kutenda kosa la kutembea na silaha mbele ya umma.

Mdee pia anakabiliwa na shtaka linguine yeye peke yake la uchochezi wa uasi huku Heche naye akikabiliwa shtaka linguine zaidi pekek yake la uchochezi wa chuki

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika Viwanja vya Buibui, wilayani Kinondon wakati wakihutubia katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Kinondoni.

Imeandikwa na James Magai, Rebecca John na Faraji Issah