Madai yatawala ndege ya Ukraine iliagushwa na kombora la Iran

Muktasari:

  •  Taarifa za Iran, viongozi wa magharibi zakinzana, uchunguzi zaidi wahitajika

Washington. Viongozi wa Canada na Uingereza wametaka uchunguzi wa kina ufanyike kubaini chanzo cha ajali iliyowaua watu 176 ndani ya ndege ya Ukraine, wakisema kuna taarifa kwamba kombora la Iran liliidungua kimakosa.

Ukraine awali ilisema inachunguza endapo ndege yake iliangushwa na kombora, jambo ambalo mamlaka za Iran zilikanusha vikali.

Kuanguka kwa ndege hiyo kulitokea saa chache baada ya Iran kushambulia kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq kwa makombora ya masafa marefu.

Maafisa wa serikali ya Marekani wakiileza televisheni ya  CBS kuwa wanaamini ndege hiyo ilidunguliwa na kombora karibu na Jiji la Tehran na kuua watu wote 176.

CBS imevinukuu vyanzo vya kijasusi vya Marekani vinavyodai kuwa picha za satelaiti zinaonyesha mwanga wa makombora mawili ambao ulifuatiwa na mwanga wa mlipuko.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema Alhamisi kuwa "nina mashaka" juu ya (kuanguka) kwa ndege. "Inawezekana kuna mtu amefanya kosa kubwa."

Iran imetangaza kutokabidhi kisanduku cheusi cha kuhifadhi taarifa za ndege kwa kampuni ya ndege ya Boeing au serikali ya Marekani kwa uchunguzi wa ajali hiyo.

Chini ya sheria za kimataifa za usafiri wa anga, Iran ina haki ya kuongoza uchunguzi wa ajali hiyo lakini kawaida huwa kampuni iliyotengeneza ndege pia hushirikishwa kwa karibu.

Na kwa mujibu wa vyombo vya habati vya magharibi, maofisa wa ujasusi wa Marekani na Iraq wana hakika kuwa ndege hiyo iliangushwa na makombora ya Iran.

Wakati CBS imechapisha taarifa inayodai kuwa mitambo ya rada ya Marekani ilibaini makombora mawili yakirushwa muda mfupi kabla ya ndege hiyo kulipuka, maafisa wawili kutoka makao makuu ya jeshi la Marekani wameithibitishia Newsweek kuwa shambulio hilo lilikuwa la bahati mbaya.

Hata hivyo, Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga wa Iran Ali Abedzadeh amesema "ndege hiyo ambayo awali ilikuwa ikielekea magharibi baada ya kupaa ilikata kona kulia kutokana na hitilafu ya kiufundi na ilikuwa ikirejea uwanja wa ndege pindi ilipoanguka."

Abedzadeh ameongeza kuwa mashuhuda waliona ndege hiyo "ikiwaka moto" kabla ya kuanguka na kuwa marubani hawakutoa taarifa yoyote ya dharura kabla ya kujaribu kurudi uwanja wa ndege wa Imam Khomeini.