Mmiliki atumia simba kulinda nyumba yake

Muktasari:

Simba huyo alipatikana akilinda nyumba pamoja na shule amekamatwa na kurejeshwa katika hifadhi.

Lagos, Nigeria. Mmiliki mmoja wa nyumba pamoja na shule ameamua kumtumia mnyama aina ya simba kwa ajili ya ulinzi.

Hata hivyo, simba huyo mwenye umri wa miezi miwili alikamatwa jana Jumatatu na kurejeshwa katika hifadhi.

Awali wakazi wa mji wa Lagos, Nigeria walipigwa na butwaa baada ya kushuhudia simba huyo akiwa katika lindo lake tofauti na ilivyozoeleka kazi hiyo kufanywa na mnyama aina ya mbwa.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la BBC, simba huyo wa miaka miwili aliripotiwa kuonekana katika nyumba moja ya makazi iliyo karibu na shule na kundi la Jopokazi Ijumaa iliyopita.

Mkuu wa Jopokazi hilo alisema kuwa baada ya taarifa hiyo, simba huyo alikamatwa na kuhamishiwa katika hifadhi ya wanyama ya Bogije Omu mjini Lekki.

“Mmiliki wa mnyama huyo ameamriwa kufika katika kituo cha polisi mara moja la sivyo atakamatwa.”

Taarifa za awali zinasema kuwa msimamizi huyo wa shule hiyo alisema kuwa walitilia maanani usalama wa watoto.

Kundi hilo linalojihusisha na masuala ya usafi wa mazingira na kitengo cha upambana na uhalifu mjini Lagos liliingilia suala hilo baada ya wakazi kuwasilisha ripoti kwa wizara ya mazingira.

Inaaminika kuwa simba huyo aliletwa katika nyumba hiyo miezi miwili iliopita.