Papa Benedict apigilia msumari sheria ya useja

Muktasari:

Amtaka Papa Francis kutolegeza kamba na kuruhusu waliooa kuwa mapadri.

Vatican, Roma. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Benedict wa 16 amesema ameshidwa kunyamaza kuhusu suala la kuruhusu wanaume walioa kutawazwa kama mapadri.

Kiongozi huyo aliyestaafu mwaka 2013 ametetea suala la mapadri kutofunga ndoa wakati ambako mrithi wake anafikiria kulegeza marufuku hiyo kwa wanaume wanaooa ambao wanahudumu kama makasisi.

Papa Benedict amesema hayo katika kitabu chake alichoandika kwa kushirikiana na Kadinali Robert Sarah.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu kutokea kwa pendekezo la kuruhusu wanaume waliooa kutawazwa kama mapadri katika eneo la Amazon.

Hata hivyo, Papa Benedict alisema katika suala hilo hawezi kunyama.

Katika kitabu hicho, Papa Benedict alisema kutofunga ndoa kwa mapadri ni utamaduni wa kale ambao umekuwapo kwa karne nyingi ndani ya kanisa hilo na kwamba una umuhimu mkubwa kwa sababu unaruhusu mapadri kufanya majukumu yao.

Papa Benedict mwenye umri wa miaka 92 alisema “halionekani kuwa jambo linalowezekana kutimiza majukumu ya upadri na ndoa kwa wakati mmoja.”

Ni nadra sana kwa Papa Benedict ambaye alikuwa wa askofu wa kwanza kujiuzulu katika kipindi cha karibia miaka 600, kuingilia masuala ya upadri.

Mara kwa mara papa huyo amekuwa akitoa maoni yake kupitia makala, vitabu na mahojiano na kutaka kiongozi wa kanisa hilo kwa sasa kuchukua njia tofauti.

Papa Benedict bado anaishi Vatican katika yaliyokuwa makao ya watawa.

Hata hivyo, Vatican bado haijasema lolote kuhusu kitabu hicho ambacho kiliandikwa kidogo katika gazeti la Ufaransa la Le Figaro kabla ya kuchapishwa leo Jumatatu Januari 13.

Wachambuzi wa Vatican wameshangazwa na hatua ya Papa Benedict kuingilia suala hilo na kuongeza kwamba hatua ya kiongozi huyo inavunja utamaduni ambao umekuwapo.

"Papa Benedict siyo kwamba anavunja ukimya wake kwa sababu hakuhisi kwamba anavunja ahadi kwa kiapo alichokula. Isipokuwa amekiuka kabisa," Massimo Faggioli, mwanahistoria na mwanatheolojia katika Chuo Kikuu cha Villanova aliandika katika mtandao wa Twitter.

Aidha, maoni ya Papa Benedikto yalielezewa kama ya kushangaza na Joshua McElwee, mwanahabari wa gazeti la National Catholic.

Nini kilichopendekezwa kubadilika katika useja wa kidini?

Oktoba mwaka jana, maaskofu wa Kikatoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia walifanya mkutano kujadiliana hatma ya kanisa hilo katika eneo la Amazon.

Katika kilele cha mkutano huo, kulitolewa ripoti yenye iliyozungumzia masuala yanayoathiri kanisa hilo na kupendekezwa kuruhusu wanaume walioa katika maeneo ya vijijini ya Amazon, watawazwe kuwa mapadri.