Putin ‘ajitosa’ mgogoro Syria

Muktasari:

  • Marais hao wamekutana katika mji wa Sochi, Urusi ili kufanikisha mpango wa kuondolewa wanamgambo wa Kikurdi katika eneo la mpaka kati ya Syria na Uturuki

Marais Recep Tayyip Erdogan (Uturuki) na Vladimir Putin wa Urusi wamekutana hii leo saa chache kabla ya kumalizika kwa muda wa makubaliano ya siku tano ya kusitisha mapigano Kaskazini mwa Syria.

Mazungumzo baina ya Rais Erdogan na Putin yaliyofanyika mjini Sochi, Urusi yanaonekana kuwa muhimu hususan katika kufanikisha mpango wa kuondolewa wanamgambo wa Kikurdi katika eneo la mpaka kati ya Syria na Uturuki.

Akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo, Rais Putin alisema “nataka kuelezea matumaini kwamba kiwango cha mahusiano kilichofikiwa kati ya Urusi na Uturuki katika nyakati hizi kitakuwa na nafasi muhimu katika suluhu ya masuala yote ya kikanda yanayojitokeza hadi sasa.”

Aidha, kwenye mazungumzo hayo Rais Erdogan ameonya kwamba ukanda huo unakabiliwa na nyakati ngumu kufuatia mzozo huo wa Syria na katika wakati ambapo muda wa kusitisha mapigano ukielekea ukingoni.

 

Rais Erdogan alisema anaamini mkutano huo utakuwa na manufaa makubwa kikanda kutokana na nyakati ngumu inazopitia. Ingawa Urusi inapingana na uvamizi wa Uturuki nchini Syria lakini kwa pamoja wanakubaliana kuanzishwa kwa ukanda salama utakaoruhusu raia kupita.

Awali, Rais Erdogan alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari kuwa “leo ni siku ya mwisho kwa wanamgambo hao kuondoka kwenye eneo hilo na kurudia kauli yake kwamba wataanzisha mashambulizi makali zaidi iwapo ahadi ambayo Marekani iliitoa kwa taifa hilo haitatekelezwa.”

Alisema atajadiliana na Rais Putin kuhusu mustakabali wa miji iliyoko mpakani ya Manbij, Qamishli na Kobane, ambayo yanaonekana ni maeneo salama yaliyopendekezwa.

Katika hatua nyingine, vikosi vya Marekani vilivyoondoka Syria vinaelekea katika nchi jirani ya Iraq ingawa Taifa hilo limesema havina ruhusu ya kukaa.

Kwa sasa Urusi imeimarisha nafasi yake katika mzozo huo  hususan baada ya Marekani kuwaondoa ghafla wanajeshi wake Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo wiki mbili zilizopita hatua iliyofungua mlango kwa Uturuki kuanzisha mashambulizi dhidi ya Wakurdi yaliyofanyika Oktoba 9.